IQNA

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei

Ubeberu kinara wake akiwa Marekani ni chanzo cha ujahili wa kisasa

10:41 - May 17, 2015
Habari ID: 3304290
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ubeberu kinara wake akiwa Marekani ndio chanzo kikuu cha kutokea ujahili wa kisasa.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran katika maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Bwana wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Waaalihi Wasallam. Kikao hicho kimehudhuriwa na  viongozi na wafanyakazi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo Iran na matabaka mbali mbali ya wananchi. Katika hotuba yake Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuhusu ulazima wa kustafidi vizuri na mafundisho yanayopatikana ndani ya mab'ath (kupewa Utume Mtume Muhammad SAW) kwa ajili ya kukabiliana kwa busara na kwa hekima ya hali ya juu na ujahilia wa kisasa ambao ni hatari zaidi kuliko ujahilia wa zama za Bwana Mtume na ambao unatumia zana za kisasa zaidi kuliko ule wa kabla ya Uislamu.  Ameutaja ubeberu wa dunia unaoongozwa na Marekani kuwa ndiyo sababu kuu ya kujitokeza ujahilia wa kisasa na kuongeza kuwa, uzoefu wa miaka 35 iliyopita wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaonesha kwamba, umma mkubwa wa Kiislamu unaweza - kwa kulinda misingi miwili mikuu wa busuri na kuona mbali pamoja na hima na nia ya kweli - kupambana vilivyo na kuushinda ujahilia huo wa kisasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu kubwa na ya kihistoria ya mab'ath kwa taifa la Iran na kwa Waislamu wote duniani na kila mtu mwenye fikra huruna kusema kwamba, mwanadamu anahitajia sana masomo na mafundisho yaliyomo ndani ya mab'ath.
Ameongeza kuwa: Kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih Wasallam kulifanyika kwa ajili ya kupambana na ujahilia; mapambano ambayo hayakuhusiana na Bara Arabu tu, bali yalihusiana na madola yote ya kijahilia ya zama hizo.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amegusia mambo mawili makuu yanayosababisha kuweko ujahilia huo ambayo ni "ufuska" na "ghadhabu" na kuongeza kuwa: Uislamu wakati huo ulipambana kwa mapana na kwa kila upande na upotofu huo katika maisha ya watu, upotofu ambao kwa upande mmoja ulitokana na hawaa za nafsi na ufuska na kwa upande wa pili ulitokana na kutawala ghadhabu, ukandamizaji na ukatili angamizi.
Vile vile amegusia kuzaliwa upya ujahilia wa kipindi cha kabla ya Uislamu katika zama za hivi sasa chini ya mambo hayo hayo mawili makuu ya ufuska na ghadhabu na kusisitiza kuwa: Hivi sasa pia tunashuhudia kuenea vitendo visivyo na mpaka na visivyodhibitika vya ufuska na ukatili na mauaji ya watu yasiyo na mipaka.
Ameongeza kuwa, tofauti baina ya ujahilia wa zama hizi na ujahilia wa kabla ya Uislamu ni kuwa, kwa masikitiko makubwa, ujahilia wa zama hizi unatumia silaha ya elimu na maarifa na hivyo ni ujahilia mbaya na hatari zaidi ikilinganishwa na ujahilia wa kabla ya Uislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Tab'an katika upande wa pili, Uislamu nao umejizatiti kwa silaha kubwa zaidi na umeweza kuenea sana duniani kwa nguvu adhimu ya Uislamu na kwa kutumia zana tofauti za kisasa na kupandisha juu matumaini ya kufanikiwa mwanadamu kuwa na mustakbali bora na kuweza mafundisho matukufu ya Kiislamu kuenea zaidi na zaidi lakini kwa sharti kwamba Waislamu wajipambe kwa sifa za busuri na kuona mbali na vile vile kwa sifa ya kuwa na nia ya kweli na hima ya hali ya juu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, hali ya hivi sasa ya nchi za Kiislamu, ukosefu wa usalama, kuuana Waislamu wenyewe kwa wenyewe, kudhibitiwa baadhi ya maeneo na makundi ya kigaidi ndani ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati ni miongoni mwa mifano ya ujahilia wa kisasa na wa leo hii ambao ni matokeo ya njama za madola ya kibeberu yanayoongozwa na Marekani na kuongeza kuwa, madola hayo yanafanya propaganda kubwa sana, tena za uongo, katika kutekeleza njama zao chafu na kulinda maslahi yao ya kibeberu na mfano wake ni pale Wamarekani wanapodai kuwa wanapambana na ugaidi.
Ameongeza kuwa, Wamarekani wanadai kupambana na ugaidi katika hali ambayo wenyewe wanakiri hadharani kuwa wamehusika katika kuunda makundi hatari kabisa ya kigaidi kama vile Daesh. Wamarekani wanaunga mkono rasmi makundi ya kigaidi nchini Syria na wanayasaidia rasmi makundi hayo. Wamarekani wanauunga mkono utawala pandikizi wa Kizayuni ambao unawashinikiza kila upande Wapalestina wa Ghaza na wa Ukingo wa Magharibi lakini pamoja na hayo wanaeneza propaganda za uongo wakidai kuwa wanapambana na ugaidi na huu kwa kweli ndio huo ujahilia wa kisasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezielekea nchi za Kiislamu na kuziambia, taifa la Iran, umma mkubwa wa Kiislamu na viongozi wa nchi za Kiislamu wanapaswa kutambua kuwa, sote kwa pamoja tunaweza kukabiliana vilivyo na ujahilia huu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja eneo kuu linalolengwa na siasa za kikhabithi za mabeberu kuwa ni eneo la Mashariki ya Kati na kwa hivi sasa siasa hizo za kibeberu zimesimama katika kushadidisha vita vya kupokezana na vya kupigana kwa niaba ya wengine.
Amesisitiza kuwa, wanachofanya mabeberu ni kutumia kila njia kufanikisha malengo yao na kuijaza fedha mifuko ya makampuni yao ya kutengeneza silaha, hivyo nchi za Mashariki ya Kati zinapaswa kuwa macho na zisikubali kuwa mateka wa siasa za madola hayo ya kibeberu.
Vile vile ametaja madai mengine ya uongo yanayoenezwa na Marekani kuwa ni madai yake kuhusiana na usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi.
Ameongeza kuwa, usalama wa Ghuba ya Uajemi unahusiana na nchi za eneo hilo ambazo zina manufaa ya pamoja na si Marekani, hivyo usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi unapaswa kulindwa na nchi zenye za eneo hilo si madola kutoka nje.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa inachojali Marekani si usalama na amani ya Ghuba ya Uajemi bali hata haina hata haki ya kutoa mitazamo yake kuhusiana na suala hilo.
Amesema: Kama eneo la Ghuba ya Uajemi litakuwa salama, nchi zote za eneo hilo zitanufaishwa na usalama huo lakini kama Ghuba ya Uajemi haitokuwa salama, nchi zote za eneo hilo nazo hazitokuwa salama.
Ayatullah Udhma Khgamenei ametaja madai mengine ya uongo ya Wamarekani kuwa ni kudai kwao kulinda usalama wa eneo hili wakati ni Wamarekani hao hao ndio waliolitumbukiza eneo hilo katika hali yake mbaya ya hivi sasa kama vile Yemen.
Ameongeza kuwa, leo hii Yemen umekuwa ni uwanja wa kuulia watoto wadogo na wanawake wasio na hatia na ingawa wanaofanya mauaji hayo ni nchi zinazodai ni za Waislamu lakini mpangaji mkuu wa mauaji hayo ni Marekani.
Amezungumzia madai mengine ya uongo ya Wamarekani za kudai kuwa eti Iran inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa, taifa la Iran limekabiliana vilivyo na ugaidi ambao ulipata nguvu nchini Iran kwa fedha na uungaji mkono wa Marekani, lakini utaiona Marekani inathubutu kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi! Wakati ambapo mtu ambaye anaunga mkono ugaidi wazi wazi ni Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa taifa la Iran litaendelea daima kupambana na ugaidi na waungaji mkono wa vitendo vya kigaidi akifafanua zaidi kwa kusema: Taifa la Iran linashirikiana na litaendelea kuwaunga mkono wale wote wanaokabiliana na magaidi hatari kabisa na Wazayuni magaidi katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon na kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia tena vitendo vya kigaidi vya Marekani na amewaelekea viongozi wa nchi hiyo akiwaambia: Nyinyi ndio magaidi. Nyinyi ndio mnaoendesha vitendo vya kigaidi. Sisi tunapinga ugaidi na tunapambana nao na tutaendelea kumuunga mkono kila anayedhulumiwa.
Ameyataja mataifa ya Yemen, Bahrain na Palestina kuwa ni miongoni mwa mataifa yanayodhulumiwa na kuongeza kuwa: Katika hali ambayo mwanzoni mwa Uislamu, washirikina wa Makka walikuwa wakisimamisha vita kwenye miezi mitukufu, leo hii tunaona kuwa huko nchini Yemen wananchi wa nchi hiyo wanamiminiwa mabomu na makombora bila ya huruma tena ndani ya mwezi wa Rajab ambao ni katika miezi mitukufu iliyo haramu kupigana vita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuwaunga mkono na kuwasaidia wanaodhulumiwa ni amri ya wazi ya dini tukufu ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Sisi tutamtetea na kumuhami yeyote anayedhulumiwa na kwa kadiri tunavyoweza na tutapambana na dhalimu kwa kiwango hicho hicho.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaka nchi za Mashariki ya Kati kuwa macho katika kukabiliana na siasa za kibeberu zinazopandikiza adui bandia ili kuzifanya nchi za eneo hili zigombane na zizozane zenyewe kwa zenyewe na kuongeza kuwa, mabeberu wanafanya njama za kuzifanya nchi za eneo hili zisimzingatie adui mkuu ambaye ni ubeberu na vibaraka wake pamoja na Wazayuni na badala yake kuzifanya nchi za Kiislamu zizozane zenyewe kwa zenyewe, hivyo inabidi tupambane vilivyo na siasa hizo tukijua kuwa huo ni katika ujahilia wa kisasa wa zama hizi.
Vile vile amesisitiza kuwa, mataifa ya eneo hili yameshaamka na kuongeza kuwa, yumkini ikatokezea wakafanikiwa kusimamisha kwa muda fulani mwamko wa Kiislamu lakini mwamko, busuri na muono wa mbali si vitu vinavyoweza kuzimwa na leo hii taifa la Iran na wananchi wa mataifa mengi ya eneo la Mashariki ya Kati wako macho na wameamka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, madola ya kibeberu kwa miaka mingi sasa yamekuwa yakifanya njama za kuzima na kukandamiza mwamko na muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati na tangu miaka 35 iliyopita, madola hayo ya kibeberu hayajasita hata mara moja kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni mhimili mkuu wa mwamko wa Kiislamu, lakini mara zote madola hayo yameshindwa na katika siku za usoni pia yataendelea kushindwa.
Kabla ya hotuba ya Kionozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Mab'ath na kukutaja kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih kwamba kulikuwa na maana ya kutia nguvu ubinadamu na kuanza kipindi kipya cha jamii ya mwanadamu yenye imani ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa mafundisho ya Mab'ath ni kwamba kitu kinachoweza kujenga historia ya mustakbali na jamii iliyopambika kwa uadilifu na usawa si upanga wala risasi na wala majengo makubwa na marefu bali ni haki na wahyi.
Aidha amebainisha kuwa, sheria aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih Wasallah kwa ajili ya wanadamu ni hekima, uadilifu, utukufu na ukamilifu wa maadili bora na kuongeza kuwa: Sheria ya Kiislamu haina uhusiano wowote na vurugu na ukatili na kwamba wale watu ambao wanataka kuihusisha sheria ya Kiislamu na vitendo vyao vya kikatili, hawajui chochote kuhusiana na sheria za Kiislamu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia njama za kueneza chuki na uhasama dhidi ya Iran katika safu za Waislamu na huku akibainisha kuwa Iran tangu zamani inapigania amani, uadilifu na kuwasaidia watu wengine amesema kuwa taifa la Iran limesimama kidete muda wote kupambana na dhulma na ubeberu na kamwe halitosalimu amri mbele ya dhulma na fikra za kupenda makuu.
Ameongeza kuwa: Iran haijawahi kuivamia nchi yoyote na katika siku za usoni pia haitofanya hivyo lakini kama itachokozwa basi itajilinda kwa nguvu zake zote kama ilivyofanya wakati wa vita vya miaka minane (vita vya kujitetea kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran).
Rais Hassan Rouhani amebainisha pia kuwa, Iran haitaki chochote zaidi ya haki zake za kisheria na amezielekea nchi za Waislamu za eneo la Mashariki ya Kati na majirani wa Iran akiziambia: Ombeni hifadhi kwenye kambi ya Bwana Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih na Qur'ani Tukufu na msiombe hifadhi kwenye kambi ya David kwani kambi pekee itakayoweza kukuokoeni ni kambi ya Bwana Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih wasallam..../em

3304067

captcha