Ujio huo bungeni ni sehemu ya shughuli zinazofanyika pembizoni mwa mashindano hayo. Washiriki hao wametembelea bunge na kuweza kukutana na kufanya mazungumzo na wabunge mbali na kufahamishwa kuhusu mfumo wa bunge hilo la Iran lijulikanalo kama Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu. Majlisi hiyo ina kamati maalumu zinazoshuhgulikia masuala ya Qur’ani.
Awamu ya 32 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Iran yalianza siku ya Ijumaa katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu nchini akiwemo Rais Hassan Rouhani.
Mashindano ya mwaka huu yanawakutanisha pamoja washiriki kutoka 120 nchi 75 duniani za mabara ya Afrika, Asia, Amerika, Ulaya na Oceania.
Pembizoni mwa mashindano hayo kutafanyika kikao cha kimataifa cha uchunguzi wa Qur'ani siku ya Alkhamisi na kutawasilishwa kazi mbalimbali zilizofanyika hadi hivi sasa katika uwanja wa Qur'ani Tukufu na namna ya kuwashawishi watu wengine kukizingatia na kukifanyika kazi Kitabu hicho Kitakatifu.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameanza sambamba na mnasaba wa Mab’ath (kubaathiwa au kupewa utume Mtume Muhammad SAW). Mashindano hayo ya kila mwaka yataendelea kwa muda wa wiki moja hadi Ijumaa tarehe 22.
Wasomi (maqarii) na waliohifadhi Qur’ani kikamilifu kutoka nchi za Kiislamu na zisizo na Kiislamu watashiriki katika mashindano hayo ya wiki moja.
Pambizoni mwa mashindano hayo ya hifdhi na kiraa ya Qur'ani, panafanyika pia duru ya 9 mkutano wa kimataifa wa utafiti wa Qur'ani unaowajumuisha wawakilishi wa zaidi ya nchi 10, vile vile kunafanyika duru ya 6 ya mkutano wa kimataifa wa kuwaenzi wanawake wanaojishughulisha na masuala ya Qurani. Halikadhalika kutakuwa na vikao 60 tofauti vya kujikurubisha na Qur'ani ambapo makari' kutoka nchini za Misri na Indonesia wanashiriki pamoja sambamba na warsha 50 maalumu za mafunzo ya Qur'ani Tukufu.../mh