Ban amesema ni jambo la kusikitisha kuwa haikuwezekana kufanya mkutano huo muhimu mapema, na amekariri wito wake kwa pande zote wa kushiriki kwenye mazungumzo hayo kwa nia njema akisisitiza kuwa suluhu ya mzozo wa Yemen ni makubaliano jumuishi ya kisiasa.
Aidha amemwomba Mjumbe wake maalum kwa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, kuahirisha mazungumzo ya amani kuhusu nchi hiyo yaliyotarajiwa kuanza huko Geneva, Uswisi tarehe 28, mwezi huu wa Mei.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban amesema uamuzi huo unafuatia ombi la serikali ya Yemen na wadau wengine kutaka muda zaidi wa kujiandaa huku akisema atajitahidi kuitisha mkutano haraka iwezekanavyo.
Akimulika hali ya kibinadamu nchini humo, Katibu Mkuu amezisihi pande zote kujali mateso ya raia wa Yemen na kushirikiana na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika utaratibu wa amani.
Tokea Saudia ianzishe hujuma zake nchini Yemen, pasina kuwepo idhini ya Umoja wa Mataifa, idadi ya waliopoteza maisha inakadiriwa kuwa Wayemen 4,000 wakiwemo watoto, wanawake na wazee. Aidha ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika misikiti, shule, hospitali, madaraja n.k. Wayemen milioni 16 kati ya milioni 25 wanahitaji misaada ya dharura kama vile chakula na dawa.
Lengo la hujuma hiyo iliyoanza Machi 26 ni kuiangusha harakati ya wananchi ya Ansarullah iliyoko madarakani na kumrejesha rais wa zamani wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi ambaye ni kibaraka wa Saudia.../mh