IQNA

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani waanza Juni 18 maeneo mengi duniani

15:09 - June 18, 2015
Habari ID: 3315879
Waislamu katika nchi nyingi duniani leo wamenza funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Taasisi husika katika nchi mbalimbali za Kiislamu na zisizo za Kiislamu zilitangaza jana jioni kwamba Alkhamisi ya leo tarehe 18 Juni itakuwa siku ya kwanza ya mwezi wenye baraka na mtukufu wa Ramadhani ambamo Waislamu hufunga swaumu na kujikurubisha kwa Mola Karima kwa kujipinda kwa ibada na dua.
Hapa nchini Iran Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilitangaza jana jioni kwamba Leo Alkhamisi ni siku ya kwanza ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo ilisema mwezi mwandamo ulionekana jana jioni na kwamba leo ni tarehe mosi Ramadhani.
Taasisi za kidini katika nchi kama Saudi Arabia, Misri, Sudan, Imarati na Qatar pia zimetangaza siku ya leo kuwa ni tarehe Mosi Ramadhani.
Leo Akhamisi pia imetangazwa kuwa tarehe Mosi Ramadhani katika nchi za Afrika Mashariki. Siku ya Jumatano Kadhi Mkuu wa Kenya Ahmed Muhdhar alitangaza kuonekana kwa mwezi kuashiria kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaanza leo. Wakati wa kutoa tangazo hilo alisisitiza umuhimu wa Wakenya kuwa na amani.
Shirika la Habari za Quran la Kimataifa IQNA linawatakia Waislamu wote mwezi uliojaa baraka wa Ramadhani na tunamuomba Mola Karima atakabali dua, ibada na amali zetu katika mwezi huu.../mh

3315350

captcha