Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hali tete ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa kuchochea mgogoro wa kimadhehebu, hitilafu, ukatili, misimamo mikali na ya kuchupa mipaka, mauaji, na Waislamu kufanywa wakimbizi ni miongoni mwa vielelezo vikuu vya hali nyeti ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati. Amesisitiza kuhusu umoja wa Waislamu ili kukabiliana na hali hiyo. Rais Rouhani ameyasema hayo hapa Tehran alipohutubu katika ufunguzi wa Mkutano wa sita wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait AS . Rais Rouhani pia amekanusha ile dhana potofu ya maadui kuwa kuna kile wanachokitaja kuwa ni 'hilali ya Kishia' wakimaanisha kuwepo nchi kadhaa katika eneo la Mashariki ya Kati zenye kufuata madhehebu ya Kishia. Amesema kile kilichopo ni ukanda wa Kiislamu.
Akijibu swali kwamba ni kwa nini maadui wanataka kuidhihirisha dini kuwa ni chanzo cha ukatili na vitendo vya kutumia mabavu, Rais Rouhani amesema dini aliyokuja nayo Nabii Mussa AS na Uyahudi ilikuwa dini ya maadili na si uvamizi ambao ni upotofu mkubwa ulioanzishwa katika dini za mbinguni na unafanya jinai kubwa huko Palestina kwa jina la dini ya Uyahudi, katika sehemu ya bara Asia unachoma moto watu kwa jina la Budha na Mashariki ya Kati baadhi ya makundi yanachinja watu na kuvunja misikiti na makanisa kwa jina la Uislamu na jihadi.
Hotuba ya Rais Hassan Rouhani katika mkutano wa leo haikuwahutubu hadhirina pekee bali ulikuwa ujumbe kwa walimwengu unaofichua hakika na sura halisi ya mirengo iliyopotoka. Katika hotuba hiyo Dakta Rouhani amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho mbele ya makundi na mirengo ambayo lengo lake ni kupotosha dini. Siasa hizi kwa hakika ni kielelezo cha kupiga ndege wawili kwa jiwe moja, kwani kama Rais Rouhani alivyosema, wakati siasa za kupiga vita na kufuta dini zilipogonga mwamba, maadui wa dini za Mwenyezi Mungu walishika mkondo mpya wa kupotosha uhakika wa dini. Ni kwa msingi huu ndiyo maana propaganda za nchi za Magharibi zikajikita zaidi katika suala la kuchafua sura ya dini na kuihusisha na ukatili na vitendo vya kuchupa mipaka.
Rais Rouhani amesema kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulibeba bendera ya dini kote duniani na kutia roho na harakati mpya katika jamii ya Kiislamu. Amesema kuwa ushindi wa Afghanistan dhidi ya Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani, kuhuishwa fikra za Kiislamu katika Mashariki ya Kati, kuanza kutolewa tena adhana katika misikiti ya Asia ya kati, mapambano ya wananchi wa Lebanon dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, harakati ya Kiislamu nchini Uturuki na katika eneo la kaskazini mwa Afrika na harakati ya mwamko wa Kiislamu kote duniani ni wimbi lililoanza sambamba na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA. Rais Rouhani amesema Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaliwatangazia walimwengu kwamba Uislamu si fikra za kuchupa mipaka bali ni imani na maadini mema. Ameongeza kuwa sauti ya Uislamu haikutangazwa duniani kwa mtutu wa bunduki bali kupitia minara ya adhana, koo na sauti za watu, misikiti, madrasa na mikutano. Amesema kuwa Uislamu ni dini ya amani, hoja na mantiki na haitumii upanga na silaha isipokuwa wakati wa dharura.
Kaulimbiu kuu ya mtutano wa sita wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait (as) ambao utaendelea kwa muda wa siku nne ni “Mshikamano na Umoja kwa Ajili ya Kupeleka Mbele Malengo ya Uislamu.” Kikao hicho kitaendelea kwa muda wa siku nne ambapo kuna washiriki 500 kutoka nchi zaidi ya 130.../mh