Dakta Ali Larijani amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini (MA) kabla ya kuondoka hapa Tehran kuelekea New York Marekani kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Maspika wa Muungano wa Mabunge Duniani. Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, nchi ambazo zinataka matatizo ya Syria na Yemen yapatiwe ufumbuzi zinapaswa kuandaa uwanja wa irada ya wananchi kuwa na nafasi katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya nchi zao. Spika Larijani amekumbusha kwamba, baadhi ya madola makubwa duniani yalikuwa na mipango ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Syria na Yemen lakini ndani ya mipango yao hiyo irada ya wananchi haikupewa nafasi na kwamba, Iran inaamini kwamba, mipango kama hiyo haiwezi kuwa na natija. Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, wananchi wanapaswa kuwa waasisi wa nchi zao na kwamba, kile ambacho kinafuatiliwa na Iran ni kuleta maafikiano na umoja wenye maana kubwa. Mkutano wa siku tatu wa Maspika wa Muungano wa Mabunge Duniani unatarajiwa kuanza Jumatatu ijayo mjini New York Marekani.../mh