Katika ujumbe wake, Rais Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika wa kitiba kwa ajili ya majeruhi wa ajali hiyo ya Ijumaa ndani ya Masjidul Haram mjini Makka. Rais wa Iran amesema ajali hiyo ya Ijumaa iliyopelekea kuaga dunia na kujeruhiwa idadi kubwa ya Mahujaji, wakiwemo raia wa Iran, ni jambo ambalo limeuumiza nyoyo za umma wa Kiislamu. Rais Rouhani sambamba na kutuma salamu zake za rambi rambi kwa waliopoteza maisha, amemuomba Mwenyezi Mungu awape afueni na shifaa ya haraka majeruhi wa tukio hilo.
Ikumbukwe kuwa jana Ijumaa alasiri zaidi ya Mahujaji 107 walipoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa baada ya kreni au winchi kuanguka ndani ya Msikiti Mkuu wa Makka. Idadi kubwa ya wafanya ziara kutoka maeneo yote duniani wanaendelea kuingia Saudi Arabia kwa ajili ya Ibada ya Hija inayotazamiwa kuanza siku chache zijazo.../mh