Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani CAIR, ambalo hutetea haki za Waislamu Marekani jana tarehe 21 Septemba lilianzisha kampeni ya kuwazawadia Wamarekani nakala za Qur'ani.
Baraza hilo limesema kampeni hiyo ni kujibu matamshi ya Carson ambaye hivi karibuni alisema kuwa Mwislamu hapaswi kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani. Akizungumza katika mahojiano na kanali moja ya televisheni siku ya Jumapili Carson pia alidai kuwa Uislamu unakinzana na katiba ya Marekani.
Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani limesema uchunguzi umebaini kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya kuwaelimisha watu kuhusu Uislamu na kuchunguza chuki dhidi ya Uislamu. Nihad Awad mkurugenzi mtendaji wa CAIR amesema, "Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani liko tayari kuitisha kikao na Carson kwa lengo la kurekebisha ufahamu wake potovu kuhusu Uislamu na atatunukiwa nakala ya Qur'ani Tukufu ili aujue Uislamu ipasavyo."
Huko nyuma CAIR iliwahi kusambaza nakala 130,000 za Qur'ani na sasa inahuisha mpango huo. Nakala za Qur'ani zinazosambazwa zina maandishi asili ya Kiarabu na tarjama ya Kiingereza pamoja na maelezo mafupi kuhusu kila aya.../mh