IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran itawatetea Wapalestina kwa uwezo wake wote

7:03 - November 26, 2015
Habari ID: 3457216
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatetea kwa uwezo wake wote harakati ya wananchi wa Palestina.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran mbele ya hadhara ya makamanda wa jeshi la kujitolea la wananchi, Basiji, ambapo mbali na kubainisha mbinu za kiadui za Uistikbari dhidi ya taifa la Iran ameongeza kuwa katika mzozo na vita halisi baina ya kambi ya Uistikbari na “kambi ya kupigania utambulisho na kujitawala” taifa la Iran litatekeleza majukumu yake ya kutetea wanaodhulumiwa hususan wananchi wa Palestina na Intifadha ya Ufukwe wa Magharibi. Huku akisisitiza kwamba Iran haiwezi kupuuza mzozo baina ya kambi ya Uistikbari na kambi ya kutetea thamani na kujitawala, Ayatullah Khamenei ameeleza kwamba misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu katika kadhia tofauti za eneo hususan suala la Palestina na masuala ya Bahrain, Yemen, Syria na Iraq iko wazi kabisa na ni ya kimantiki. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria utendaji wa vyombo vya habari vya Kiistikbari kuhusiana na kadhia ya Palestina na kufafanua kwamba: wao wanawaita magaidi watu wanaorusha mawe kulalamikia kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na kubomolewa nyumba zao; lakini wanawaunga mkono wale watu wanaoyaharibu maisha na heshima ya Wapalestina. Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria pia kadhia ya Bahrain kwa kueleza kwamba takwa pekee la wananchi wa nchi hiyo ni la kuwa na haki ya kupiga kura na akaongezea kwa kusema: kundi dhalimu la watu wachache linawatawala wananchi hao na kuyavunjia heshima matukufu pamoja na maombolezo ya Muharram ya wananchi hao wa Bahrain. Ayatullah Khamenei amezungumzia pia mashambulio ya mtawalia yanayowaandama wananchi wa Yemen na akasema: katika hali kama hii vyombo vinavyodai kutetea demokrasia na haki za binadamu vinawaunga mkono watu wanaowalenga wananchi wa Yemen kwa hujuma za mashambulio. Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuhusiana na mgogoro wa Syria kwamba wananchi wenyewe wa Syria ndio wenye haki ya kuamua juu ya mustakabali wa nchi yao…/

captcha