IQNA

Waislamu 21 wa madhehebu ya Shia wauawa Shahidi Nigeria

23:35 - November 27, 2015
Habari ID: 3457492
Waislamu 21 wa madhehebu ya Shia wameuawa shahidi katika jimbo la Kano, kaskazini mwa Nigeria baada ya gaidi moja kujiripua kwenye msafara wa Waislamu hao Ijumaa hii.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine wengi wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo la kigaidi.
Shambulizi hilo limetokea katika kijiji cha Dakasoye kilichoko umbali wa kilomita 20 kusini mwa mji wa Kano wakati Waislamu wa Shia walipokuwa kwenye msafara wa kutembea kwa miguu katika barabara ya Kano-Zaria kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein AS. Sheikh Muhammad Turi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria amesema mashambulizi hayo ya kigaidi hayatawazuia Waislamu wa madhehebu ya Shia kutekeleza shughuli zao za kidini. "Hata kama watatupiga sisi sote kwa mabomu, hatutaacha kutekeleza shughuli zetu za kidini hadi atakapouawa mtu wa mwisho", amesema Muhammad Turi.

Ikumbukwe kuwa takribani miaka 1376 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) akiwa na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi za siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.
Kundi la kigaidi la Boko Haram linatuhumuwa kuhusika na hujuma hiyo. Ingawa hadi sasa kundi hilo halijadai kuhusika lakini katika siku za huko nyuma limekuwa likitekeleza mashambulizi kama hayo sio tu dhidi ya Mashia lakini pia dhidi ya Waislamu wa Kisuni na hata Wakristo nchini Nigeria.

3457478

captcha