Akizungumza Ijumaa katika kikao cha Baraza la Uratibu na Mipango la mkoa wa Khorasan Razavi katika mji Mtakatifu wa Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran, Rais Rouhani ameongeza kuwa, kwa bahati mbaya hii leo mashambulizi ya kigaidi yamefungua njia ya hujuma za kipropaganda dhidi ya Uislamu na Waislamu; katika hali ambayo magaidi na jinai wanazofanya hazina mahusiano yoyote na Uislamu au Qur'ani.
Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa, magaidi wanajiarifisha kuwa ni Waislamu na kitendo hicho ndicho kinachopelekea fikra za waliowengi duniani kutoa hukumu na maamuzi yasiyo sahihi kuhusu dini Tukufu ya Uislamu na Waislamu. Akiendelea na hotuba yake, Rais wa Iran ameameshiria pia uchaguzi wa baraza linalomchagua Kiongozi Muadhamu na ule wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge hapo tarehe 26 mwezi Februari mwakani na kuongeza kuwa, vyombo vyote vinafanya juhudi ili kuandaa mazingira mazuri na ya utulivu ili chaguzi hizo zifanyike kwa ufanisi.