IQNA

Mwanamke aliyevaa Hijabu atimuliwa mkutano wa kampeni Marekani

10:19 - January 10, 2016
Habari ID: 3470029
Polisi nchini Marekani wamemtimua mwanamke Mwislamu aliyevalia Hijabu ambaye alikuwa katika mkutano wa kampeni uliokuwa ukihutubiwa na Donald Trump anayewania kupata tiketi ya chama cha Republican kugombea urais nchini humo.

Rose Hamid, 56, siku ya Ijumaa alikuwa katika mkutano wa kampeni wa Trump kwa lengo la kulalamikia hatua ya mwanasiasa huyo tajiri kutoa matamshi yaliyo dhidi ya wakimbizi Waislamu kutoka Syria.

Trump alipomuona Bi. Hamid aliwataka polisi wamtimue kutoka katika mkutano huo.

Baada ya kutimuliwa katika mkutano huo wa kampeni, Bi. Hamid alisema alifika katika mkutano huo ili kuwaonyesha washiriki taswira halisi ya mwanamke Mwislamu. Ameongeza kuwa alisimama wakati wa mkutano huo ili ampe Trump na wafuasi wake fursa ya kumuona mwanamke aliyevalia Hijabu. Ameongeza kuwa wafuasi wa Trump walimzingira na kumvunjia heshima kama mwanamke mwislamu.

Kufuatia hujuma za kigaidi za Paris, Ufaransa na San Bernardino Marekani, Trump alitaka Waislamu wasiruhusiwe kukanyaga ardhi ya Marekani. Msimamo huo mkali wa Trump amepelekea kuibuka wimbi jipya la chuki dhidi ya Uislamu Marekani. Aidha mwanasiasa huyo anayewania kuwa rais wa Marekani alitaka kutumiwe mbinu za manazi wa Ujerumani chini ya uongozi wa Adolph Hitler dhidi ya Waislamu.

3465921

captcha