
Watu wasiopungua saba wameuawa Alhamisi asubuhi na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya miripuko ya mabomu kuutikisa mji wa Jakarta.
Msemaji wa Polisi Anton Charliyan amesema miongoni mwa waliopoteza maisha katika hujuma hiyo ni raia watatu na afisa wa polisi.
Rais wa nchi hiyo, Joko Widodo ameitaja miripuko hiyo kama shambulio la ugaidi na kuagiza wahusika kusakwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kwa mujibu wa polisi ya Indonesia, miripuko hiyo imetokea nje ya jengo moja la kibiashara linaloitwa Sarinah Mall katika kitovu cha Jakarta. Kadhalika milio ya risasi imesikika katika eneo hilo, muda mfupi baada ya miripuko hiyo.
Kundi la kigaidi la ISIS limedai kupitia mitandao ya kijamii kuwa limehusika na hujuma hizo za mji mkuu wa Indonesia lakini madai hayo hayajaweza kuthibitishwa.
Habari zaidi zinasema kuwa, eneo hilo lenye shughuli nyingi lina mahoteli ya kifahari, balozi na afisi nyingi za serikali na za binafsi.
Itakumbukwa kuwa, watu 202 waliuawa katika shambulio kubwa la ugaidi lililowahi kuikumba nchi hiyo mwaka 2002 katika eneo la kitalii la Bali.