
Kwa mujibu wa tovuti ya Akhbar Sudan, Rais Bashir ameyasema hayo Jumatano usiku wakati wa kufungwa Awamu ya 7 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani nchini Sudan.
Rais Bashir amesema Qur'ani Tukufu inaweza kutatua matatizo ya leo duniani kama vile dhulma, mauaji na misukosuko. Aidha amesema, "Kwa kuzingatia mafundisho ya Qur'ani kutapatikana njia ya kuukomboa mji wa Quds na kuunda umma moja wa Kiislamu."
Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Sudan ambayo pia yanajulikana kama 'Zawadi ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Khartoum yalikamilika Januari 10.
Mashindano hayo yalifanyika katika kategoria tatu ambazo ni kuhifadhi Qur'ani kikamilifu pamoja na tafsiri ya Juzu 24 kwa wanaume, kuhifadhi Qur'ani kikamilifu kwa wanawake, na kuhifadhi Juzuu tatu za Qur'ani kwa washiriki kutoka nchi zisizo za Kiislamu.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwakilishwa katika mashindano hayo na Ali Assadi ambaye alishiriki katika kategoria ya kuhifadhi Qur'ani kikamilifu.