
Kauli hiyo imetolewa na Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisheria na kimataifa alipokuwa akizungumza katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OI)C huko Jeddah, Saudi Arabia. Aidha amesisitiza kwamba, jumuiya hiyo imenyamazia kimya changamoto kubwa hususan kadhia ya Palestina lakini imechukua hatua ya haraka mno kuhusiana na kushambuliwa ubalozi wa Saudia mjini Tehran.
Abbas Araqchi ameashiria hatua zilizochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya tukio la kuvamiwa ubalozi wa Saudia mjini Tehran mapema mwezi Januari na kubainisha kuwa, Iran mbali na kulaani kitendo hicho imeanzisha uchunguzi wa kina kwa ajili ya kuwatambua waliohusika na uvamizi huo ili mkondo wa sheria ufanye kazi yake na kwamba, muda sio mrefu matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa.
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonyesha kusikitishwa kwake na hatua ya OIC ya kuitisha haraka kikao cha dharura kujadili suala hilo, ililahi ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu Palestina ilipoomba kuitishwa kikao cha dharura cha OIC ili kujadili mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa lakini hadi leo ombi halijashughulikiwa.