
Jason Cone, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) nchini Marekani katika makala katika mtandao wa gazeti la Time amesema pia kuwa wanajeshi wa Saudia wamekuwa wakiwalenga raia katika mashambulio yao huko nchini Yemen.
Afisa huyo wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka ameongeza kuwa, inaonekana kuwa, kuwalenga raia na miundo mbinu ya Yemen ni katika malengo ya vikosi vya Saudia huko Yemen.
Jason Cone ameashiria pia mashambulio ya anga ya Saudia huko Yemen dhidi ya taasisi hiyo ya utoaji misaada ya kibinadamu. Amesema, masuala yote hayo yanabainisha na kuweka wazi ukiukaji wa wazi kabisa wa sheria za vita na kinga ya kisheria ya taasisi na wafanyakazi wa masuala ya kitiba.
Saudia na waitifaki wake waliivamia Yemen mwezi Machi mwaka uliopita na takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa karibu watu 8,400 wameuawa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa huku makumi ya maelfu ya wengine wakiachwa bila makazi.
Wengi wa wahanga wa hujuma za Saudi Arabia nchini Yemen ni raia wakiwemo wanawake na watoto wadogo. Aidha Saudia mbali na kulenga mahospitali pia imekuwa ikidondosha mabaomu katika misikiti, shule, madaraja na maghali ya maji kwa lengo la kuwalazimisha wananchi wa Yemen watii matakwa yake haramu.