
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu aliyasema hayo Jumatano asubuhi mjini Tehran aliponana na Admeli Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza
Kuu la Usalama wa Taifa pamoja na manaibu na wataalamu wa sekretarieti
ya baraza hilo. Huku akiashiria namna istilahi na neno "usalama"
lilivyo tata na lilivyo na vipengee vingi tofauti katika dunia ya leo,
amelitaja jukumu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa ni kufanya
maamuzi kwa kuangalia upana na vipengee vyote vya neno usalama na kwamba
jukumu kuu la sekretarieti ya baraza hilo ni kuandaa maamuzi ya
kuonesha njia sahihi ya uchukuaji maamuzi ndani ya Baraza Kuu la Usalama
wa Taifa. Amesisitiza kuwa: Ili sekretarieti hiyo iweze kutekeleza
vizuri na kwa njia sahihi nafasi muhimu sana ya kuandaa maamuzi, inabidi
anga iliyopo katika sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na
mikakati yake ikubaliane kikamilifu na "fikra sahihi, halisi na safi ya
kimapinduzi na ya kihizbullah (ya mtu aliyeko kwenye chama cha Mwenyezi
Mungu yaani aliyeshikamana vilivyo namafundisho ya dini)."
Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, usalama ni moja
ya mambo ya kimsingi zaidi na ya lazima zaidi katika jamii na ni kwa
sababu hiyo ndio maana Qur'ani Tukufu imelizungumzia mara nyingi suala
hilo. Ameongeza kuwa: Leo hii suala la usalama limetoka katika sura yake
ya kuishia tu kwenye masuala ya kijeshi na kiusalama na lina upeo pia
wa masuala ya kiuchumi, kimaisha, kiutamaduni, kisiasa, kijamii,
kisaikolojia na kimaadili.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja jukumu
kuu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kwamba ni kuwa na mtazamo mpana
kuhusu kadhia ya usalama na kuzingatia vipengee vyake vyote. Ameongeza
kuwa: Sekretarieti ya baraza hilo inapaswa kutekeleza vizuri mno wajibu
wake mkuu wa kuandaa maamuzi kwa namna ambavyo misimamo inayochukuliwa
na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa iwe inachukuliwa kutokana na kuwa na
mtazamo sahihi unaozingatia pande zote za neno usalama.
Vile vile
amegusia kazi tofauti za sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa
na kusema kuwa: Suala la sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa
ya kuweza kutekeleza kwa njia sahihi majukumu yake, linategemea kutawala
kikamilifu anga ya asilimia mia moja ya kimapinduzi katika chombo hicho
kwani kama misimamo inayokinzana na misimamo ya Mapinduzi ya Kiislamu
itajipenyeza kwenye suala la uandaaji wa maamuzi katika sekretarieti ya
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, basi matunda yanayotakiwa hayataweza
kupatikana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza
kuwa, misimamo ya kimapinduzi si fikra chapwa zisizo na lolote ndani
yake na kuongeza kuwa: Misimamo ya kimapinduzi ni jambo la kweli lililo
wazi na wadhiha kikamilifu na ni lenye msingi wake katika matamshi ya
Imam (Khomeini) Rahimahullah.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia jinsi
baadhi ya watu wanavyojaribu kubadilisha njia na mipaka ya asili na ya
wazi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Imam - Mwenyezi Mungu
amrehemu - ndiye dhihirisho la Mapinduzi ya Kiislamu na kwa msingi huo,
matamshi yake yaliyokusanywa kwenye jalada kadhaa za kitabu cha "Misingi
ya Mapinduzi" ndiyo marejeo mipaka hiyo.
Amesema, mambo
yaliyokaririwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika matamshi yake
hayo ni mipaka na mistari mikuu na ndiyo misingi ya Mapinduzi ya
Kiislamu na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa matamshi ya Imam - Rahimahullah
-suala la "wananchi," "uhuru wa nchi," "kushikamana na dini na misingi
ya Uislamu," "kupambana na uistikbari na ubeberu," "kadhia ya
Palestina," "suala la maisha ya wananchi," "kuwazingatia wanyonge na
kutokomeza umaskini" ndiyo misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo
yanapokusanyika pamoja yanajenga muundo mkuu na halisi wa Mapinduzi ya
Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia
kuwa, maamuzi ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa yanapaswa kuwa ndani ya
fremu ya misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa:
Inabidi fikra sahihi na halisi ya kimapinduzi na "kihizbullah" itawale
kikamilifu ndani ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na sekretarieti ya
baraza hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tangu mwanzoni
kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuna baadhi ya watu
walikuwa hawakubaliani na fikra ya kimapinduzi, na kwamba baadhi yao,
licha ya kwamba walikuwemo ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini
walikuwa hawaitakidi kuwa kuna haja ya kupambana na ubeberu na
uistikbari; sasa inabidi kusimama imara kukabiliana na watu wenye
misimamo kama hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amesisitiza kuwa, mapambano yamekuwepo katika kipindi chote cha miaka 37
iliyopita, hata hivyo lakini amesema: Tab'an, leo hii mapambano hayo
yamekuwa nyeti mno na magumu zaidi kutokana na mbinu mpya na tata mno
zinazotumiwa na adui kama vile kutumia mitandao ya kijamii na
kujipenyeza katika masuala ya kiutamaduni, kiitikadi, kijamii na mambo
mengine yaliyo dhidi ya amani na usalama wa taifa.
Ayatullah Udhma
Khamenei ameashiria pia jinsi mbinu mpya zinazotumiwa na maadui
zinavyoathiri pole pole na kimya kimya misingi ya ndani kabisa ya
usalama katika jamii na kuongeza kuwa: Baraza Kuu la Usalama wa Taifa
lina wajibu wa kufuatilia masuala yote hayo katika sekta tofauti na
hatimaye kuyachukulia maamuzi na ndio maana sekretarieti ya baraza hilo
inapaswa kuwa na tafakuri sahihi na kufanya juhudi zisizochoka na za
kiutaalamu zilizosimama juu ya msingi wa fikra ya kimapinduzi na baadaye
kuandaa maamuzi sahihi ya kuweza kukabiliana vilivyo na mbinu tata na
mpya za adui wa usalama na amani ya taifa.
Mwishoni mwa hotuba yake,
amemtaja Admeli Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa
ni miongoni mwa kumbukumbu nzuri sana za kipindi cha vita vya kujihami
kutakatifu (Vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani
wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran) na ameishukuru sekretarieti ya baraza hilo kutokana na jitihada na
kazi zake nzuri za kuandaa ripoti muhimu na za wakati mwafaka kuhusiana
na maudhui tofauti.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa
Taifa ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za sekretarieti ya baraza hilo na
kusema kuwa, kupanga sera, kuratibu na kusimamia ndiyo majukumu makuu ya
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa nchini. Ameongeza kuwa, sekretarieti ya
baraza hiyo ina jukumu la kuunga mkono na kusaidia kiutaalamu maamuzi wa
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na kwamba nafasi hiyo daima inapaswa
ioane na iwe katika mkondo wa siasa kuu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu
na za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
3472675