
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tovuti ya Sumeria imeripoti Ijumaa hii kuwa, Adnan Al Fahdawi, mwanachama wa Baraza la Mkoa wa Al Anbar Iraq amesema sala ya Ijumaa imehudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa pamoja namaafisa wa ngazi za juu serikalini. Ameongeza kuwa: "Mji wa Ramadi Ijumaa hii umeshuhudia sala ya kwanza ya Ijumaa ya umoja wa Mashia na Masunni kwa mara ya kwanza tokea mji huu ukombolewe kutoka kwa magaidi wa ISIS (Daesh).
Jenerali Yahya Rasul , msemaji wa oparesheni ya vikosi vya Iraq alitangaza tarehe 27 Desemba mwaka 2015 kuwa mji wa Al Ramadi umekombolewa kutoka mikonini mwa magaidi wa ISIS na bendera ya Iraq kupeperushwa katika mji huo.
Wiki iliyopita pia Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni Iraq katika wilaya ya Al Mikdadiya mkoani Diyala nchini Iraq wamesali pamoja sala ya Ijumaa. Zayyid Al-Azzawi mkuu wilaya ya Al Mikdadiya alisema kuwa lengo la kusaliwa sala hiyo ni kusisitiza umoja wa Waislamu na kukurubisha zaidi madhehebu za Kiislamu katika eneo hilo ili kukabiliana na wanaolenga kuibua fitina za kimadhehebu.