IQNA

Wafanyakazi uwanja wa ndege Paris marufuku kuwa na nakala za Qur'ani!

11:23 - May 23, 2016
Habari ID: 3470329
Wafanyakazi Waislamu katika Uwanja wa Kimatiafa wa Ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, Ufaransa wamekatazwa kuwa na nakala za Qur'ani wakiwa kazini huku wanaokataa kunyoa ndevu wakichukuliwa hatua.

Maafisa wa usalama wa Ufaransa wanadai wamechukua hatua hizo kufuatia hujuma za kigaidi mjini Paris katika miezi ya Januari mwaka huu na Novemba mwaka jana. Hivi sasa wafanyakazi wote Waislamu katika viwanja vya ndege kote Ufaransa wanachunguzwa na vyombo vya usalama kuhusu misimamo yao ya kidini.

Katika ukaguzi uliofanyka katika uwanja wa ndege wa Charels de Gaulle, wakuu wa usalama wamebatilisha asilimia 60 ya vibali vya wanaoruhusiwa kuwa katika eneo la kuegeshea ndege. Imearifiwa kuwa vibaki hivyo vimebatilishwa kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni 'tabia zisizofaa'.

Waislamu walipokonywa vibali wanadaiwa kuswali katika baadhi ya misikiti ambayo maafisa wa usalama wanaamini huwa na hotuba zenye misimamo mikali. Aidha wafanyakazi wanaume ambao wanakataa kuwapa mkono wafanyakazi wa kike nao pia wamepokonywa vibali vya kali.

Usalama umeimarishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Charles de Gaulle, baada ya ndege ya Misri ya Shirika la EgyptAir kuangika katika bahari ya Mediterranean Alkhamisi ikitokea uwanja huo wa ndege.

Wakuu wa Misri wamedokeza kuwa yamkini ndege hiyo ilianguka kutokana na bomu lililokuwa ndani na hivyo kuwepo uwezekano kuwa wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle walihusika na kuanguka ndege hiyo.

Kufuatia kukithiri vitendo vya kigaidi Ufaransa, kumeibuka wimbi kubwa la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya.

captcha