Watu 8 wauawa katika hujuma dhidi ya Msikiti
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, hujuma hiyo ilijiri Jumapili usiku katika msikiti ulio katika kambi ya wakimbizi ya Azerni katika kile kinachotajiwa ni mapigano ya kikabila.
Kufuatia mauaji hayo ndani ya msikiti, maelfu ya wakaazi wa eneo hilo wameandamna kulaani kuuawa watu waliokuwa wakiswali ndani ya msikiti katika mji huo wa El Geneina ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Darfur Magharibi.
Wakati wa mazishi ya waliouawa ndani ya msikiti kulifanyika maandamano makubwa huku waandamanaji wakitaka gavana wa eneo hilo afutwe kazi.
Serikali ya Sudan bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu na tukio hilo.
Mrengo wa upinzani unaamini kwamba, hatua ya serikali ya Sudan ya kuligawa eneo la Darfur katika maeneo matatu hapo mwaka 1994 na kisha kuligawa tena katika majimbo matano baadaye, ulikuwa mwanzo wa kuibuliwa machafuko ya mwaka 2003 sanjari na kushadidisha udhibiti wa serikali katika majimbo hayo.
Mapigano katika eneo la Darfur yanahusisha makabila ya wabeba silaha yanayoituhumu serikali ya Khartoum kwa kufanya ubaguzi dhidi yao. Mapigano hayo hadi sasa yamesababisha zaidi ya watu laki tatu kuuawa na zaidi ya wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.