IQNA

Nukta za kipekee katika uongozi wa Imam Khomeini MA

12:00 - June 02, 2016
Habari ID: 3470353
Ijumaa hii Wairani na wapenda haki duniani wanakumbuka siku ya kufariki dunia Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikuwa na nuktaa za kipekee katika uongozi wake.

Miaka 27 iliyopita, yaani tarere 3 Juni 1989 Milaadia, wananchi wa Iran walitumbukia kwenye majonzi na huzuni kubwa kufuatia kufariki dunia Imam Khomeini MA ambaye kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu aliweza kuleta mapinduzi makubwa katika uongozi wa Iran kwa kuyafikisha kwenye ushindi mapinduzi hayo matukufu yenye sifa za kipekee duniani. Baada ya ushindi wa mapinduzi hayo, Imam Khomeini aliasisi mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran na kuuongoza mfumo huo wa utawala kwa muda wa muongo mzima katika kipindi kigumu na nyeti mno kilichojaa mawimbi ya matukio mazito ya ndani na uadui wa kila upande wa mabeberu.
Imam Khomeini MA aliweza kuulinda utawala huo mchanga wa Iran kwa muda wa miaka minane kwenye vita vya kidhulma visivyo na mlingano sawa lilivyolazimishwa kupigana taifa la Iran. Wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, uwezo, ukakamavu na umakini wa Imam Khomeini ndiyo siri ya kudumu na kuendelea kuwepo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa na tamaa kwamba kwa kufariki dunia Imam, kungelizuka mizozo na mivutano ya kuwania madaraka ya kisiasa ndani ya Iran na kuvuruga mshikamano wa kitaifa na kisiasa wa wananchi wa Iran. Lakini tamaa hizo za maadui zimeedelea hadi leo hii kuwa njozi zisizoagulika kwani katika kipindi hicho nyeti cha historia ya Iran, Baraza la Wanavyuoni Wataalamu la Kumchagua na Kusimamia Kazi za Kiongozi Muadhamu lilifanya haraka kumchagua Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei kuchukua nafasi ya Imam kuyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ililivuusha salama taifa la Iran katika kipindi hicho nyeti na hatari sana. Hivi sasa na baada ya kupita miaka 26 ya tangu kufariki dunia Imam Khomeini MA, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa imara na yenye nguvu kubwa zaidi ikiendelea kwa nguvu zake zote katika njia ya kufanikisha malengo yake matukufu. Leo tumemua kuzungumzia mada hii tuliyoipa jina la Sifa za Kipekee za Kifikra na Kisiasa katika Uongozi wa Imam Khomeni ili kuona ni kiasi gani dunia ya leo hususan ulimwengu wa Kiislamu uliotumbukia kwenye mizozo mikubwa ya kimadhehebu; unavyoweza kutumia fikra za mwanachuoni huo kujikwamua kutoka kwenye hali nzito uliyomo ndani yake hivi sasa.
Katika kipindi cha karne moja iliyopita, kumetokea mapinduzi mengi katika nukta tofauti duniani. Baadhi ya mapinduzi hayo yamefikia ushindi kamili lakini Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanatofautiana na mapinduzi yote hayo kutokana na kuwa kwake na kiongozi mwenye fikra za aina yake na za kipekee yaani Imam Khomeini MA. Tofauti na viongozi wa mapinduzi mengine duniani, Imam Khomeini ni marja'a na mwanachuo mkubwa wa kidini. Umuhimu wa sifa hiyo unazidi kuonekana wakati tunapozingatia kipindi yalipofikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, yaani katika kipindi ambacho dunia ilikuwa inatawaliwa na kambi mbili kubwa za dunia, kambi ya kikomunisti na ile ya kibepari. Fikra ya kwanza iliyokuwa ikitawala wakati huo duniani ni ya mapinduzi ya Kimaksi ambayo inapinga dini kikamilifu na aidiolojia hiyo ilitumika kuwanyonya wanyonge. Fikra nyingine ni ile ya kiliberali na kibepari ambayo inaitoa dini kikamilifu katika masuala ya kisiasa na inatilia mkazo mifumo ya kisekula na kilaiki kwa ajili ya kuendeshea masuala ya kisiasa na kijamii badala ya dini ingawa inaamini kuweko Mwenyezi Mungu. Lakini Imam Khomeini MA aliongoza Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuuthibitishia ulimwengu kuwa, dini tukufu ya Kiislamu si tu haiwanyonyi wanyonge na madhlumina, lakini pia inapinga dhulma kwa sura zake zote kama ambavyo pia inaona mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu ni jambo la dharura katika masuala ya kisiasa, kijamii, kupigania ukombozi, uhuru, uadilifu wa kijamii na umaanawi katika jamii na haiwezekani kuutenganisha Uislamu na mambo hayo.



Sifa nyingine ya kipekee iliyomo kwenye uongozi wa kisiasa za kimapinduzi wa Imam Khomeini ni kutegemea nguvu zisizokwisha na zisizoshindika za Mwenyezi Mungu na kutawakali Kwake. Imam aliongoza harakati za mapinduzi katika kipindi ambacho wanafikra na wachambuzi wote wa mambo duniani walikuwa wanasema kwamba ilikuwa ni muhali kuupindua utawala wa kiimla na kidikteta wa Shah uliokuwa umejiimarisha kwa kila namna. Imam Khomeini aliichagua aidiolojia ya Kiislamu kuwa njia bora kabisa ya kupambana na utawala huo wa ukandamizaji na kufanikiwa kuwahamasisha wananchi wa Iran kusimama na kupambana na utawala wa kidikteta na kitaghuti wa mfalme Shah. Imam aliongoza mapambano dhidi ya utawala ambao uliokuwa umejizatiti kikamilifu kwa silaha na kupata uungaji mkono wa kila upande wa madola ya kibeberu. Cha kuvutia zaidi ni kuwa, Imam Khomeini aliongoza mapambano hayo katika wakati ambapo licha ya kambi mbili zilizokuwepo wakati huo zilizokuwa zinaongozwa na Urusi ya zamani na Marekani duniani na ambazo zilionekana kupingana katika baadhi ya mambo, lakini zote wakati huo zilikuwa zinauunga mkono utawala wa kiimla wa Shah nchini Iran. Imam Khomeini aliingia kwenye mapambano hayo akiwa mikono mitupu na silaha yake pekee aliyokuwa nayo ilikuwa ni kutawakali na kuelekeza matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu na kwenye nguvu za wananchi. Imam Khomeini alikuwa na yakini ya kupata ushindi kwa kutegemea nguvu zisizoshindika za Mwenyezi Mungu na nguvu kubwa za wananchi. Tofauti na makundi mengine ya kisiasa ya zama hizo ambayo yalikuwa na fikra ya kuendesha vita vya silaha kama njia ya kuingia madarakani, Imam aliamini kuwa nguvu za wananchi wa matabaka yote zitakapounganishwa pamoja na kutumiwa vizuri kwa kutegemea taufiki ya Mwenyezi Mungu, huwa hakuna nguvu yoyote inayoweza kupambana na nguvu kama hizo za wananchi.
Imam Khomeini alikuwa na welewa wa kina kuhusu masuala na matukio ya wakati wake pamoja na matukio ya kihistoria. Tangu akiwa kijana, Imam Khomeini alikuwa anafuatilia kwa karibu matukio ya ndani ya Iran na ya kimataifa na kwamba utambuzi na welewa wake huo mkubwa na mpana wa mambo ulimsaidia sana katika kuchukua maamuzi muhimu, ya kihistoria na yenye taathira kubwa.


Fikra za Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi zilijengeka juu ya misingi ya mahitaji ya kihistoria ya wananchi wa Iran tangu wakati wa mapambano ya kupigania mfumo wa sheria nchini Iran na pia malengo matukufu ya wasomi wanaoangalia mbali wa Iran na wa dunia nzima katika zama zake. Kuunganishwa pamoja mambo yote hayo kulisaidia mno katika kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwa mfano msimamo wa Imam Khomoeini wa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Paletina na msimamo wake wa kuupiga vita utawala wa Kizayuni msimamo ambao ulionekana kwa wingi mno ndani ya maneno yake, ulionesha ni kiasi gani alikuwa na muono wa mbali kwani kadiri siku zinavyopita ndivyo usahihi wa msimamo huo wa Imam Khomeini unavyozidi kudhihirika. Suala la kulitetea taifa madhulumu la Palestina ni katika matakwa na malengo matakatifu ya wananchi wa Iran. Suala hilo lilikuwa linafuatiliwa kwa hisia kali pia na wasomi wa dunia na wananchi wote wa nchi za Kiislamu na Kiarabu na wote hao walimsifu na kumshukuru Imam Khomeini na taifa la Iran kwa kuwa na msimamo kama huo wa kupigiwa mfano.
Sifa nyingine ya kipekee ya fikra ya kisiasa na kimapinduzi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni sisitizo la Imam Khomeini MA kuhusu udharura wa kushikamana na kuwa kitu kimoja Waislamu bila ya kujali madhehebu yao. Msimamo huo wa kihistoria na kidini ndiyo yaliyokuwa malengo matukufu ya wapigania marekebisho wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu kuanzia Jamaluddin Asad Abadi hadi Dk Ali Shariati ambao lengo lao kuu lilikuwa ni kuwarejeshea Waislamu hadhi na heshima yao. Imam Khomeini alikuwa mlinganiaji mkubwa wa kuhuishwa Uislamu na kushikamana Waislamu katika mapambano yao dhidi ya dhulma za ndani ya ulimwengu wa Kiislamu na za mabeberu wanaoingilia masuala ya ulimwengu huo. Imam hakusisitiza suala la mshikamano na umoja wa Waislamu katika maneno tu, bali alitekeleza kivitendo suala hilo na hilo ndilo linalompambanua Imam Khomeini na wapiganiaji wengine wa marekebisho ndani ya ulimwengu wa Kiislamu. Imam Khomeini alikuwa mstari wa mbele katika kupigania jambo hilo na alikubali kuingia katika hatari kubwa kwa ajili ya kulinda na kupigania kishujaa malengo hayo matakatifu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Mapinduzi ya Kiislamu yakapata umaarufu mkubwa na yakatoa taathira za kustaajabisha katika mwamko wa Kiislamu kwenye nchi za Kiislamu.


Sifa hizo maalumu na za kipekee tulizoziashiria kwenye makala hii fupi ni sehemu ndogo tu ya sifa za kipekee alizokuwa nazo mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sifa hizo ndizo zilizopelekea Mapinduzi ya Kiislamu kupata ushindi nchini Iran na Jamhuri ya Kiislamu kuwa imara hadi leo hii. Hivi tunavyoiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni imara zaidi leo hii baada ya kupita miaka 36 ya tangu kuasisiwa kwake, sababu ya jambo hilo limetokana na sifa hizo za kipekee kama vile kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu na za wananchi, kuwatetea wanyonge na watu wanaodhulumiwa, kutoogopa vitisho vya kigeni, kuhimiza na kutilia mkazi umoja na mshikamano wa Waislamu bila ya kujali madhehebu yao kwa ajili la kuhuisha adhama na utukufu wa Uislamu na Waislamu na sifa nyinginezo kama hizo.
Amma kuongezeka nguvu na ushawishi wa Iran katika ulimwengu wa Kiislamu na duniani kote kwa kutegemea fikra za Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu kumewafanya maadui wa Uislamu na Iran wazidishe njama zao tata na za kila aina. Leo hii maadui wa Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu wameanzisha makundi yanayomkufurisha kila mtu katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuupaka matope Uislamu mbele ya fikra za walimwengu. Maadui hao wanafanya njama za kuyaimarisha, kuyakuza na kuyatia nguvu makundi hayo ya kitakfiri kama njia ya kupambana na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujaribu kufuta sifa ya mapenzi, huruma, kupigania haki, uhuru na kuheshimiana iliyojikita ndani ya dini tukufu ya Kiislamu.
Mataifa yanayodhulumiwa duniani hususan ya Waislamu yanapaswa kuwa macho mbele ya njama hizo hatari za Kimarekani na Kizayuni kwani matokeo ya jinai zinazofanywa na makundi hayo ya kigaidi na kitakfiri si kitu kingine ila kudhamini maslahi ya Magharibi, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hivyo jambo ambalo linaweza kuyaokoa mataifa yanayodhulumiwa kutokana na ubeberu na uingiliaji wa kigeni pamoja na dhulma na ukosefu wa uadilifu, ni fikra za Mapinduzi ya Kiislamu zilizomo kwenye tafakuri na aidiolojia ya mwasisi wa mapinduzi hayo matukufu, Imam Khomeini MA.



captcha