IQNA

Khatibu wa Saala ya Ijumaa Tehran

Siku ya Quds ni ya kupambana na Mzayuni, adui mkuu wa Uislamu

20:11 - July 01, 2016
Habari ID: 3470426
Khatibu wa Saala ya Ijumaa Tehran amesema Siku ya Kimataifa ya Quds ni hatua kubwa kupambana na uistikbari na adui Mzayuni aambaye ndiye adui mkuu wa Uislamu.
Akizungumza katika hotuba za Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran, Ayatullah Ahmad Khatami amewashukuru wananchi wa Iran kwa hatua yao ya kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa Quds yaliyofanyika leo kote ulimwenguni na kueleza kuwa: "Njama za maadui wa Uislamu za kuipuuza kadhia ya Palestina na Quds Tukufu kamwe hazitafanikiwa kutokana na kuwa macho na kusimama kidete Waislamu hususan wananchi wa Palestina."

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameendelea kusema kuwa, umma wa Kiislamu ni umma mmoja na ulioshikamana na kuongeza kuwa: Waislamu ulimwenguni kote hawatanyamaza kimya madhali wananchi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wangali katika makucha ya utawala ghasibu wa Kizayuni.

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa Tehran amesema kuwa, ni karibu miaka sabini sasa wananchi wa Palestina wanaendelea kushikiliwa katika jela la utawala wa Kizayuni na kwamba Wamagharibi hususan Marekani ndio walioasisi kundi la Daesh ili kuzipotosha fikra za walio wengi kuhusu kadhia ya Palestina huku wakighafilika kuwa umma wa Kiislamu kamwe hautaruhusu walimwengu waisahau kadhia ya Palestina.

Ayatullah Khatami amesisitiza kuwa, Palestina itaendelea kuwa moja ya masuala ya kimataifa na Kiislamu na haiwezi kubadilika na kuwa kadhia ya Wamagharibi. Ayatullah Khatami amesisitiza kuwa ni kwa sababu hiyo ndio maana maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kila mwaka hufanyika kwa hamasa kubwa zaidi.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika jiji la Tehran aidha amesema, Marekani inaeneza madai ya uongo ya kwamba eti inapigania haki za binadamu na kupamba na ugaidi, katika hali ambayo nchi hiyo yenyewe ni muungaji mkono mkuu wa ugaidi; na wala haionyeshi radiamali yoyote ya kukabiliana na jinai zinaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Ahmad Khatami ameelezea kusikitishwa na mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni huko Istanbul Uturuki na kusema kuwa, chanzo cha matatizo hayo yote ni uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo kwa kundi la kigaidi la Daesh. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitahadharisha kwa mara kadhaa nchi zinazolifadhili kundi la Daesh kwamba kuna siku jinai za kundi hilo zitakuja kuzidhuru pia nchi hizo zinazoliunga mkono.

 3511772
captcha