IQNA

Sala ya Ijumaa Tehran

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: Matembezi ya Arubaini ni shughuli ya kiroho ya aina yake

21:26 - September 15, 2023
Habari ID: 3477604
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa Tehran hii leo amesema matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) ni zoezi la kimaanawi la aina yake na lisilo na mfano.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo leo katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa hapa Tehran na kueleza kuwa, matembezi ya Arubaini ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu, na ambao ni wa aina yake na usio na mfano wake duniani.

Ayatullah Khatami amebainisha kuwa, Arubaini (Arbaeen) ya Imam Hussein (AS) ni harakati mashuhuri katika utamaduni wa kisiasa wa Iran na dunia. Amesema licha ya Mazuwari zaidi ya milioni 22 wakiwemo Wairani milioni 4 kushiriki katika Arubaini ya mwaka huu, lakini vyombo vya habari vya Wamagharibi vilikataa kuakisi tukio hilo kutokana na hamaki zao.

Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran ameongeza kuwa, Arubaini ndio harakati kubwa na mashuhuri zaidi dhidi ya ubeberu na uistikbari katika dunia ya leo.

Kadhalika amewashukuru viongozi wa serikali ya Iran na Iraq kwa maandalizi waliyoyafanya kwa ajili ya maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) mwaka huu.

Septemba 6 iliyosadifiana na tarehe 20 Safar mwaka 1445 Hijria, ilifanyika kumbukumbu ya Arubaini ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa Waislamu wa madhehebu Shia na wafuasi wake waaminifu katika jangwa la Karbala, nchini Iraq mwaka 61 Hijria.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa Tehran hii leo amesema adui anajaribu kuvunja umoja wa taifa la Iran, lakini amesisitiza kuwa, Wairani kwa kufuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, wataendelea kushikamana na kusimama kidete dhidi ya maadui.

Ayatullah Khatami ameashiria mkutano wa Jumatatu iliyopita wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alipoonana na wakazi wa mikoa miwili ya "Sistan na Baluchistan" na ule wa "Khorasan Kusini" na kubainisha kuwa, kikao hicho kiliwaghadhabisha mno maadui.

4169082

Habari zinazohusiana
captcha