
Taarifa zinasema May anatazamiwa kuendeleza sera zake dhidi ya Waislamu akiwa katika nafasi ya kiongozi wa Uingereza.
May ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani alichukua hatamu za
uongozi Uingereza siku ya Jumatano kutoka kwa David Cameron na ameahidi
kupambana na kile alichokitaja kuwa ni misimamo mikali kwa kustawisha
thamani na mila za Uingereza hasa uhuru wa maoni.
Hii ni haki ambayo aliwapokonya wanachuo Waislamu katika vyuo vikuu vya
Uingereza mwezi Novemba mwaka 2014 wakati alipopendekeza Sheria ya
Kukabiliana na Ugaidi. Sheria hiyo ambayo ilipitishwa katika bunge la
Uingereza iliwazuia wanafunzi Waislamu kubainisha mitazamo yao katika
mihadhara na semina kwa hofu ya kutajwa kuwa wenye misimamo mikali.
Wakati May akiwa waziri wa mambo ya ndani, Waislamu Uingereza
waliandamwa na kupelelelzwa na maafisa maalumu wa polisi waliotumwa
katika mitaa yao. Ni kwa sababu hii ndio mwaka jana Tume ya Haki za
Binadamu za Kiislamu ikamtaja May kuwa 'Mtu Mwenye Chuki Dhidi ya
Uislamu katika Mwaka' au Islamophobe of the Year.
Waislamu Uingereza wanakubaliana kwa kauli moja kuwa, vitendo vya May
akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alipelekea chuki na hujuma dhidi ya
Waislamu kuwa kitu cha kawaida katika jamii na matokeo yake ni kuwa hali
inazidi kuwa mbaya kwa Waislamu milioni tatu nchini Uingereza.
3514951