IQNA

Chakula Halali Rio chawavutia hata wasiokuwa Waislamu

11:45 - August 15, 2016
Habari ID: 3470524
Mgahawa Halali ulio katika makao ya wanariadha katika michezo ya Olimpiki huko Rio de Janeiro nchini Brazil mbali na kuwavutia wanariadha Waislamu pia unawavutia wasiokuwa Waislamu.

Mgahawa huo katika Kijiji cha Olimpiki Rio unasimamiwa na Kituo cha Kiislamu cha Brazil kwa ajili ya kuhakikisha wanariadha Waislamu na maafisa wengine Waislamu katika Olimpiki wanapata chakula halali.

Akizungumza na mwandishi wa IQNA, mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Brazil Hujjatul Islam Sheikh Khazraji amesema mgahawa huo unatoa aina mbali mbali ya chakula cha Kiarabu, Kitaliano, Kiasia n.k.

Amesema mgahawa huo wa chakula halali uko wazi kwa Waislamu n ahata wasiokuwa Waislamu wanaoshiriki katika michezo ya Olimpiki.

Sheikh Kazraji amesema Kituo cha Kiislamu cha Brazil kimewahi kusimamia utayarishaji wa chakula Halali nchini Brazil katika mashindano ya Kombe la Soka Duniani ya FIFA mwaka 2014 na pia katika Kikao cha Umoja wa Mataifa cha Maendeleo Endelevo (Rio + 20).

Kituo cha Kiislamu cha Brazil kilitayarisha mapendekezo maalumu kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kuhusu kuhakikisha Waislamu wanaoshiriki katika michezo ya Olimpiki Rio de Janeiro wanapata chakula kilichotayarishwa kwa msingi wa Uislamu.

Kwa mujibu wa taarifa, kutakuwa na milo 65000 kwa siku kwa ajili ya wanariadha 18,000 ambapo milo 8000 itakuwa maalumu kwa ajili ya Waislamu huku ikiwa na nembo ya Halal.

Uislamu uliingia Brazil kwa mara ya kwanza kupitia watumwa kutoka Afrika na kisha kutoka wahamiaji wa Lebanon na Syria na inakadiriwa kuwa Waislamu ni asilimia moja hivi ya watu wote milioni 162 katika nchi hiyo.

3460690

captcha