IQNA

Wahubiri wa Kiwahhabi wapigwa marufuku Misikitini Misri

8:09 - October 30, 2016
Habari ID: 3470643
IQNA-Serikali ya Misri imewapiga marufuku wahubiri wa Kiwahhabi kuhutubu hotuba katika misikiti ya nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Awqaf ya Misri imeeleza kuwa, Mawahabi (Masalafi) hawana ruhusa ya kuhutubia katika misikiti ya nchi hiyo na kwamba, shakhsia wenye idhini ya kutoa hotuba katika misikiti ya nchi hiyo ni wale maulama wanaochaguliwa na Kituo cha Kiislamu cha al-Azhar.

Aidhaa taarifa hiyo imesisitiza kuwa, matamshi yanayonasibishwa na Mkuu wa Awqaf katika mji wa Damietta ya kutoa idhini kwa Mawahabi kuhutubia katika misikiti ya nchi hiyo hayana ukweli wowote.

Katika sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Awqaf ya Misri inaeleza kuwa, makhatibu na watoa waadhi wenye idhini ya kuhutia katika misikiti ya Misri ni wale wanaoteuliwa miongoni mwa Maulama wa al-Azhar na wanapata idhini ya kufanya hivyo baada ya kupitia kozi ya lazima.

Hatua hiyo ya Wizara ya Awqaf ya Misri inatahminiwa na wajuzi wa mambo kwamba, inalenga kukabiliana na misimamo ya kufurutu ada na hotuba za kichochezi ambazo zimekuwa zikitolewa na Masalafi wa Kiwahabi nchini humo.

Takwimu zinaonyesha kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh au ISIS linaloyakalia maeneo kadhaa ya ardhi za Syria na Iraq limevutia vijana wengi kutoka nchi za kaskazini mwa Afrika zikiwemo Tunisia, Libya na Misri. Vijana hao hushawishika kutokana na mitazamo ya kufurutu mpaka ya Kiwahabi.

Wakati huo huo, mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Kiislamu cha Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha nchini Misri amesem akuwa, hivi sasa dini tukufu ya Kiislamu imekumbwa na mashambulizi ya kila upande ya maadui na yote hayo yanatokana upotoshaji wa watu unaofanywa na baadhi ya makundi yenye welewa potofu kuhusu Uislamu.

Sheikh Muhyiddin Afifi aidha ameutahadharisha sana umma wa Kiislamu na viongozi wa Misri akiwaambia kuwa, hivi sasa mashambulizi ya maadui dhidi ya Uislamu yameongezeka.


captcha