Kabla ya hapo muda muda wa kuwepo walowezi wa Kizayuni kila siku katika Msikiti wa Al Aqsa ulikuwa kuanzia saa moja na nusu hadi saa nne asubuhi. Mpango huu ni katika fremu ya utawala wa Kizayuni kuugawa Msikiti wa Al Aqsa kwa mujibu wa kile kinachotajwa kuwa ‘mahala na wakati’
Kwa mujibu wa taratibu mpya Wazayuni sasa watakusanyika katika msikiti huo kuanzia saa moja na nusu hadi saa tano asubuhi. Katika mkusanyiko woa huo wa kila siku katika uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa, Wazayuni hutekeleza ibada ya Kiyahudi zijulikanazo kama Talmud.
Uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni ni katika fremu ya njama za hatua kwa hatua ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa miezi kadhaa katika msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.
Mwaka uliopita, utawala wa Kizayuni ulianzisha rasmi taratibu ya kuugawa Msikiti wa Al Aqsa kwa zama au wakati ambapo Wazayuni wanapata masaa kadhaa ya kuwepo katika msikiti huo. Hivi sasa muda wa Wazayuni kuwepo katika msikiti huo umeongezwa jambo ambalo ni ukiukwaji wa wazi wa haki za Waislamu. Mbali na utawala wa Kizayuni kutekeleza ukiukwaji huo hivi sasa pia wakati wa sherehe za Kiyahudi, Waislamu hawataruhusiwa kuingia katika Msikiti wa Al Aqsa.
Jumla ya siku hizo ni 200 kwa mwaka ambapo Mayahudi hawatawaruhusu Waislamu kuingia katika Msikiti wa Al Aqsa.
Kimsingi kwa mujibu wa mpango huo, Wazayuni wanaweza kutumia kisingizio chochote kile kuwazuia Waislamu kuingia katika msikiti huo wakati wowote ule.
Katika njama ya kuuagawa Msikiti wa Al Aqsa kwa mahala, utawala wa Kizayuni unadai kuwa maeneo yenye paa katika msikiti huo ni ya Waislamu na maeneo yasiyo na paa yanahesabiwa kuwa ya Mayahudi.
Kwa msingi huo asilimu 60 ya eneo la Msikiti wa Al Aqsa linatambuliwa na utawala wa Kizayuni kuwa milki ya Wazayuni.
Kwa kuzingatia mipango ya ujenzi na ramani bandia walizonazo Wazayuni, inatabiriwa kuwa, iwapo mpango wa kuugawa Msikiti wa Al Aqsa utatekelezwa kikamilifu kutaibuliwa maeneo mengi bandia yatakayopewa majina ya Kiyahudi katika eneo la msikiti huo na natija ya hilo hatimaye itakuwa ni kutekelezwa njama ya kuubomoa kikamilifu msikiti huo ambao ni eneo la tatu kwa utukufu katika Uislamu.
Mpango huo unatekelezwa huku tayari kukiwa na mradi wa kuchimba njia za chini kwa chini; chini ya Msikiti wa Al Aqsa tokea eneo hilo likaliwe kwa mabavu. Kujenga chini ya msikiti ni dalili ya wazi kuwa lengo la mwisho la Wazayuni ni kuubomoa msikiti huo na kujenga mahala pake hekalu bandia la Suleiman.
Wanadai hekalu hilo lilikuwa hapo tokea zama za kale lakini nyaraka zilizotegemewa zote ni bandia na za kujibunia bali hata kuna nyaraka ambazo zimethibtisha dai hilo kuwa ni la uongo.
Uchochezi huo wa Wazayuni katika Msikiti wa Al Aqsa bila shaka utakuwa mwanzo wa hujuma mpya dhidi ya Wapalestina na kuenea machafuko zaidi katika eneo hilo.
Waplestina wameutaka umma wa Kiislamu kuchukua hatua za haraka za kuuhami na kuulinda msikiti wa al-Aqsa na njama za utawala wa Kizayuni.