Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, harakati ya mapambano ya Palestina ilisema kuwa walowezi waliingia kwa nguvu katika viwanja vya msikiti huo wa Kiislamu na kufanya “matendo ya kichokozi” huku wakilindwa na wanajeshi wa Israel.
Hamas ilieleza kuwa uvamizi huo wa karibuni ni “sehemu ya juhudi za kukata tamaa za utawala wa Israel kuufuta kabisa utambulisho wa Kiislamu na Kiarabu” wa eneo hilo takatifu.
“Tukiwa tunashuhudia uvamizi huu unaozidi na kurudiwa mara kwa mara, ni wazi kwamba huu ni mpango wa kimfumo wa kuuyahudisha msikiti, na njama hii inaendeshwa na utawala dhalimu wa kibeberu,” taarifa hiyo ilisoma.
Hamas iliwaomba Wapalestina wote walioko katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu waungane kwa sauti moja kupinga “njama hizi za kifashisti zinazolenga ardhi yao na maeneo yao matakatifu.”
Mamia ya walowezi wa Kiyahudi waliuvamia Msikiti wa Al-Aqsa, ulioko katika Mji Mkongwe wa al-Quds, siku ya Jumatatu asubuhi, katika kile kilichoonekana kama uchokozi wa wazi unaoendelea kufanywa katika eneo hilo takatifu.
Idara ya Waqfu wa Kiislamu iliripoti kuwa zaidi ya walowezi 500 waliingia katika msikiti huo kwa makundi, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya Israel.
Makundi ya walowezi hao waliingia kupitia Lango la Wamoroko (Babul Maghariba), lililoko upande wa Magharibi wa Haram al-Sharif, wakiandamana na polisi wa Israel waliokuwa na silaha nzito.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina, Wafa, walowezi kadhaa pia walionekana wakifanya ibada za Kiyahudi za Talmudi na kucheza ngoma za kichokozi karibu na milango kadhaa ya kuingilia msikiti wa Al-Aqsa.
Waqfu wa Kiislamu ulionya kuwa Msikiti wa Al-Aqsa unakabiliwa na ongezeko kubwa la ukiukwaji unaofanywa na walowezi wa Kiyahudi na vikosi vya polisi wa Israel. Ukiukwaji huo ni pamoja na: Uvamizi unaozidi wa walowezi hao, kuongezeka kwa idadi ya walowezi wanaoingia kwa pamoja, kuongezeka kwa ibada za Talmudi zinazofanywa ndani ya viwanja vya msikiti na vyote vikifanyika chini ya ulinzi wa majeshi ya Israel.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Israel na serikali ya Jordan baada ya uvamizi wa Israel katika al-Quds mwaka 1967, ibada za dini zisizo za Kiislamu katika msikiti huo haziruhusiwi. Hata hivyo, marufuku hiyo ni ya maneno tu, kwani kwa vitendo hali imekuwa kinyume kabisa na haki za Waislamu.
Uvamizi huu wa kichokozi katika Msikiti wa Al-Aqsa unafanyika wakati Israel inaendeleza mashambulizi ya kikatili katika Ukanda wa Gaza.
Tangu mwaka 2003, Israel imekuwa ikiwaruhusu walowezi kuingia katika eneo hilo la msikiti karibu kila siku.
Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, Hamas ilitoa wito kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kuchukua hatua za haraka na madhubuti kusitisha kampeni ya mauaji ya halaiki inayoendeshwa na Israel dhidi ya watu wa Gaza walioko kwenye mzingiro.
/3493315