IQNA

Mtume Muhammad SAW, Kigezo cha Umoja wa Waislamu

8:20 - December 17, 2016
Habari ID: 3470746
IQNA-Waislamu duniani wanasherehekea Maulidi na kukumbuka tukio la kuzaliwa Mbora wa Walimwengu, Muhammad Mwaminifu SAW. Ni fusa muafaka ya kutafakari kuhusu umoja wa Waislamu duniani.

Kipindi cha baridi kali cha zama za ujinga na ujahilia cha dunia kilikuwa kikihesabu miaka, miezi saa na dakika kikisubiri kuingia msimu wa machipuo ya Rabiu Awwal kwa shabaha ya kupata uhai mpya wa nuru na mwanga wa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu. Wakati huo alikuja Ahmad Msifiwa na kuhuisha dunia iliyokuwa imegubikwa na kiza totoro. Alihuisha nafsi za wanadamu waliokuwa katika ujinga na ujahili kwa kaulimbiu ya laa ilaha illallah (hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki illa Allah Mmoja) na kuziita kuelekea kwenye ukamilifu wote chini ya bendera ya Tauhid.
Naam. Wakati huo alikuja Muhammad akiwa tabibu wa roho za wanadamu na uturi wenye harufu nzuri kwa dunia iliyokuwa imeghiriki katika ukatili, ujinga, na maovu yote. Aliwalingania watu wote kuwa ndugu na kuwataka waishi kwa wema bila ya kujali hitilafu zao za kimaumbile.

Kwa kauli ya Ahul Sunna, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku mwaka 570 Miladia huku wanachuoni wa madhehebu ya Shia wakiamini alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huo huo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Wiki ya Umoja wa Waislamu

Umoja wa Waislamu una maana ya wafuasi wa dini hiyo kushikamana na kuishi pamoja kwa amani na kukabiliana kwa pamoja na hatari zinazokabili dini yao na jamii ya Waislamu kwa kushikamana na mambo yanayowakutanisha pamoja kama Qur'ani', Tauhidi, Suna za Mtume, na Mtukufu huyo mwenyewe. Umoja wa Waislamu una maana ya kujiepusha na hitilafu mbalimbali za kimadhehebu, kisiasa, kimbari, kilugha na kadhalika. Udharura wa kuwa na umoja kati ya Waislamu unaongezeka zaidi na zaidi katika kipindi cha sasa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Uislamu na Waislamu wanalengwa zaidi katika zama hizo kuliko kipindi kingine chochote na kunafanyika mipango chungu nzima ya kusambaratisha Waislamu na dini yao. Hivyo basi ni wajibu kwa Waislamu wote wanaofuata amri za Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Qur'ani tukufu kutekeleza sira na mwenendo wa maisha wa mtukufu Mtume tunayesherehekea kuzaliwa kwake katika kipindi hiki. Mtume huyo ambaye aliweza kuibadili jamii ya kijahili iliyokuwa ikijifaharisha kwa vita, ukatili kama ule wa kuzika watoto wadogo wa kike wakiwa hai na kadhalika na kuifanya umma mmoja wenye nguvu elimu na mshikamano.

Mtume Muhammad SAW alizingatia suala ya Umoja

Mtume Muhammad SAW alilipa umuhimu mkubwa suala la umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Baada tu ya kuhamia Madina, mtukufu huyo alifanya mikakati kabambe ya kuwapa izza na heshima Waislamu. Miongoni mwa mbinu zilizotumia na mtukufu huyo ni kufunga mikataba ya kujenga udugu baina ya makundi mbalimbali yaliyokuwa yakihasimiana kwa miaka mingi. Mikataba hiyo iliunga udugu baina ya makundi mbalimbali hasimu ya Madina, baina ya watu wa Madina na wahajiri kutoka Makka na hata baina ya makabila ya Aus na Khazraj ambayo yalikuwa vitani kwa kipindi cha zaidi miaka mia moja. Mtume SAW alielewa kwamba Uislamu hauwezi kukita mizizi katika maeneo ambako watu wana hitilafu za kikaumu, kimbari, kimatabaka na kijamii. Hivyo alichukua uamuzi wa kuunga udugu baina yao. Kazi hiyo ya kuunga udugu baina ya Waislamu ilifikia kiwango cha Mwislamu kumtanguliza Mwislamu mwenzake mbele ya nafsi yake mwenyewe. Historia inahadithia kuwa, wakati wa kugawa ngawira za vita, Mtume SAW aliwaambua Ansar ambao walikuwa watu wa Madina kwamba kama mnataka mnaweza kuwahirikisha Muhajirina waliokuwa wahajiri kutoka Makka katika ngazwira, au uchukua ngawira zote nyinyi peke yenu. Ansari walisema: Tunawapa ngawira zote ndugu zetu Muhajirina na na tutagawana na kuwapa sehemu ya mali na nyumba zetu. Kwa hakika hatua ya Mtume ya kujenga udugu baina ya Muhajirina na Ansari ilijenga umoja usio na kufani baina ya makundi hayo mawili ya Waislamu.

Umoja ulikuwa miongoni mwa sababu kuu za izza, heshima na ushindi wa Waislamu wa awali katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Kinyume chake migawanyiko na mifarakano hauna matokeo ghairi ya kuharibu rasilimali za Umma wa Kiislamu na kuutumbukiza katika madhila na udhaifu. Ili kuimarisha umoja na mshikamano wa wa Umma wa Kiislamu Mtume SAW alipiga vita kwa maneno na matendo vitendo vyote vya ubaguzi, fikra za kwatenga na kuwagwa watu kulingana na kaumu na makabila yao na kadhalika. Ili kuthibisha hayo kimatendo alimteua Zaid bin Haritha aliyekuwa mtumwa na kumfanya kamanda wa Jeshi la Uislamu na akamteua Bilal al Habasi, mtumwa mweusi kutoka Afrika kuwa muadhini wake muhtasi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kigezo cha utukufu katika Uislamu na mafundisho ya Mtume SAW ni takwa na uchamungu.

Mtume SAW alipiga vita taasubi za kimbari, kikaumu na kimakundi

Vilevile imepokewa kwamba siku moja Salman Farsi alikuwa ameketi msikitini pamoja na masahaba wengine wa Mtume SAW baadhi ya masahaba walianza kuzungumzia asili, fasili na nasaba zao huku kila mmoja akitaja fahari ya nasaba na asili yake. Ilipofika zamu ya Salman Farsi maswahaba walimtaka ataje nasaba na asili yake. Swahaba huyo mwema ambaye alikuwa mwanakikiji kutoka uajemi yaani Iran ya sasa, badala ya kutaja na kujifaharisah kwa asili na nabasa yake alisema kuwaambia maswahaba: Naitwa Salman mana wa mja mmoja wa Mwenyezi Mungu. Nilikwua nimepotea mwenyezi Mungu akaniongoa kupitia kwa Muhammad. Nilikuwa fakiri na maskini, mwenyezi mungu akanitosheleza kupitia kwa Muhammad. Nilikuwa Mtumwa mwenyezi Mungu akanifanya huru kupitia kwa Muhammad. Hii ndiyo asili na nasaba yangu. Wakati huu Mtume SAW aliingia msikitini hapo na akapewa ripoti ya yote yaliyojiri. Mtume SAW aliwageukia maswahaba zake na kuliambia kundi la watu ambao wote walikuwa Maquraish kwamba: Enyi Maquraish! Damu ina maana gani! Na mbali ina thamani ipi! Nasaba na fahari ya kila mtu ni dini yake. Uungwana wa mtu ni tabia njema, ufahamu na uelewa wake sahihi na uchapakazi, na hakuna asili na nasaba bora kuliko akili." Hivi ndivyo Mtume SAW alivyopiga vita taasubi za kimbari, kikaumu na kimakundi na kujenga msingi wa umoja na mshikamano wa Kiislamu.

Katika jitihada zake za kupiga vita taasubi na chuki hizo za kikabila ya kimbari, Mtume Muhamamd SAW alikuwa akiwasaidia na kuwa karibu sana na watu waliokuwa wakidhulumiwa ambao aghlabu yao walikuwa watumwa wasiokuwa na himaya ya kabila au kaumu za Madina. Kwa sababu hiyo tu watu hao walikuwa wakinyimwa haki zao zote za kisiasa, kijamii na kadhalika. Mtume aliwaambia kwamba wanadamu wote ni sawa katika maumbile yao na kwamba wote wana roho, hisia na maumbile ya kibinadamu licha ya tofauti zao za kirangi, kimbari, kikabila au utaifa ambavyo hazipisi kuwa sababu ya ubaguzi katika haki.

Mtume SAW alitumie hekima kujenga udugu

Katika upande mwingine mtukufu huyo alielewa kwamba kufuta na kung'oa fikra iliyokita mizizi katika fikra na akili za watu sawa wawe mabwana au watwana katika kipindi cha maelfu ya miaka kulihitajia mapinduzi makubwa ya kiutamaduni. Hii ni kwa sababu watumwa walikuwa wamepoteza kabisa nguvu ya irada na kujichukulia maamuzi kutokana na ada ya miaka mingi na mabwana hawakufirikia kabisa kwamba watuwma wao wana haki sawa na zao za kisiasa, kijamii na kadhalika. Mtume SAW alitumia hekima yake isiyo na kifani kujenga jamii yenye udungu wa Kiisalmu katika mazingira hayo na kuwaweza kuwafundisha "mabwana" na 'watwana" kuwa wote ni ndugu katika Uislamu na kwamba wote wanatokana na asili moja ambayo ni udongo. Alisisitizia kuwa wanadamu wote ni sawa kama meno ya magego licha ya tofauti katika rangi, kaumu na maeneo yao.
Hapana shaka kuwa zama za sasa, wapenzi wasikilizaji zinahitajia sana sira na mafundisho ya Mtume Muhammad (saw) katika kuvumiliana, kupendana na kustahamili mitazamo inayotofaitiana ni yetu. Vilevile tunapaswa kuiga sira ya Mtume SAW kuhusu jinsi ya kuwa macho na njama za maadui wanaolenga umoja na mshikamano wa Waislamu ambao jiwe lake la msingi liliwekwa na mtukufu huyo mwenyewe.

captcha