IQNA

Kumbukumbu ya kuaga dunia Mtume Muhammad SAW

"Nimetumwa ili kuja kukamilisha maadili bora"

22:48 - September 24, 2022
Habari ID: 3475833
IQNA-Mwezi 28 Mfunguo Tano Safar, inasadifiana na siku ya kukumbuka alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW.

Siku kama hii mwaka wa 11 Hijria, Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al Mustafa, SAW alitangulia mbele ya Haki akiwa ametekeleza vilivyo jukumu alilopewa na Mola wake Mlezi. Bwana Mtume Muhammad SAW ni rehema kwa walimwengu wote na lengo la ujumbe wake alilifupisha kwenye maneno yafuatayo: "Nimetumwa ili kuja kukamilisha maadili bora."

Tunaitumia fursa hii kutoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW na tunachukua fursa hii kuangazia muhtasari sira iliyojaa baraka ya mtukufu huyo, tukimuomba Mwenyezi Mungu ayajaalie haya machache tunayoyazungumza hapa, yawe ni utangulizi wa kuziamsha akili zetu na kujipamba kwa sifa bora za mtukufu huyo.

Bwana Mtume Muhammad SAW alitumwa kwa walimwengu katika kipindi ambacho dunia ilikuwa imejaa ujahili, dhulma na utovu wa uadilifu. Katika kipindi hicho cha kiza totoro, alidhihiri mtukufu huyo akiwa na maneno bora kabisa yenye mvuto wa kipekee kwa walimwengu wote. Aliwaambia :  Semeni: "Hakuna Mungu ila Allah, mtafuzu". Yaani enyi wanadamu mliozongwa na ujinga na ujahili, shirki na ukosefu wa uadilifu, semeni: Hakuna Mungu ila Mungu Mmoja tu, naye ni Allah, mjisalimishe Kwake ili mupate kufuzu duniani na Akhera.
Bwana Mtume alikuja na dini aali na bora kabisa kwa ajili ya wanadamu, yaani Uislamu, chini ya kivuli cha maneno hayo yaliyojaa nuru.

Amma swali linalojitokeza hapa ni kuwa, vipi baada ya kuweko yote haya mazuri yaliyojaa nuru ndani ya Uislamu, linatokezea kundi la watu linaathiriwa na takataka za mghafala na chuki za roho na kutenda ukatili na mambo ya kijahilia na kuyanasibisha na Uislamu wakati hayana uhusiano wowote na dini tukufu ya Kiislamu? Hivi kwani, si kwa baraka za risala ya Bwana Mtume Muhammad SAW ndipo ulipozimwa moto wa vita na mauaji ya wenyewe kwa wenyewe; na watu wote wakawa kitu kimoja wakaishi kwa kuhurumiana chini ya kivuli cha Uislamu? Hivi kwani si ni kwa baraka za maadili mema ya Bwana Mtume Muhammad SAW ndipo nyoyo za watu zililainika na kuvutika kwake? Bwana Mtume aliweza - chini ya kivuli cha Uislamu - kuwabadilisha watu waliokuwa na misimamo mikali mno wa enzi za ujahilia huko Bara Arabu, kuwa wapole, wema na wanaohurumiana si baina ya wao kwa wao tu, bali pia baina yao na watu wa dini nyinginezo na si baina ya wanadamu kwa wanadamu tu, bali waliheshimu pia haki za viumbe wengine hata miti.

Maadili Bora ya Bwana Mtume SAW

Wema na maadili bora kama hayo hayakuwahi kuhushudiwa mithili yake kabla ya kudhihiri Bwana Mtume Muhammad SAW na dini tukufu ya Kiislamu. Ni jambo lililo wazi kuwa, kuua maelfu ya watu wasio na hatia, wanawake na watoto wadogo na vizee na viajuza kwa madai kuwa watu hao wanafuata madhehebu na dini nyinginezo, ni mambo ya kikatili ambayo yanakinzana kikamilifu na mafundisho matukufu ya Uislamu na sira iliyojaa nuru ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa hakika ukatili unaofanywa na magenge ya kigaidi unatokana na mghafala, ujinga na ukatili binafsi wa magenge hayo, na hauna uhusiano wowote na dini tukufu ya Kiislamu.

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, vipi tutaweza kuutambua Uislamu wa kweli? Kuisoma kwa kina sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW, ni moja ya njia za kuutambua Uislamu wa kweli. Swali jengine la kujiuliza ni vipi wanatokezea baadhi ya Waislamu wanadanganyika na kutumbukia kwenye jinai za zama za kijahilia? Ni katika sehemu gani ya maisha ya Bwana Mtume iwe ni kabla ya Uislamu au baada ya Uislamu, panapoonekana matendo kama hayo maovu na ya ajabu? Inasikitisha kuona kuwa makundi hayo ya watu yanatumia hadithi za uongo na kuzinasibisha kwa Bwana Mtume ambaye ni mbora wa viumbe kwa umbo na kwa tabia. Vitendo hivyo vinapingana kikamilifu na sira ya mtukufu huyo wa daraja ambaye ni rehema kwa walimwengu wote. Wigo wa mapenzi na huruma za Bwana Mtume Muhammad SAW ni mkubwa na mpana sana kiasi kwamba ziliwaenea watu wote, kuanzia mtu wake wa karibu mno hadi kwa masahaba wake na pia kwa watoto wadogo, mayatima na hata wasio Waislamu. Ni kwa sababu hii ndio maana katika wakati wa minasaba kama hii ya kukumbuka siku alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW, huwa tunamuomba Mwenyezi Mungu aziepushe nyoyo zetu na mighafala na atupe nguvu za kufuata Uislamu wa kweli uliofundishwa na mtukufu huyo wa daraja kwa amri ya Mola wake Mwingi wa rehema.

Sira ya Mtume ni Njia ya Kuufahamu Uislamu

Kama tulivyotangulia kusema, kuitambua vyema sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW ni moja ya njia za kuutambua Uislamu wa kweli. Katika kuwalingania watu Uislamu, Bwana Mtume alikuwa na msimamo usiotetereka lakini aliupamba msimamo huo kwa huruma na mapenzi. Kwa maneno mengine ni kuwa, Bwana Mtume alioanisha kwa njia nzuri sana maneno na matendo yake, na kuifanya sira yake tukufu iache taathira kubwa katika nyoyo za watu. Tunapoiangalia sira ya mtukufu huyo tunaona kuwa, njia kuu aliyoitumia kuwalingania watu Uislamu ilikuwa ni hoja na kulea moyo wa kutafakari na kutia mambo akilini.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana ujumbe wa awali kabisa wa mtukufu huyo ukawa ni umuhimu wa elimu na dini. Bwana Mtume SAW alikuwa akiwalingania watu kujipinda kwa elimu na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa maarifa na umtambuzi sahihi. Wakati Bwana Mtume alipobaathiwa na kupewa Utume, Waarabu walikuwa wakiishi katika ujahilia mkubwa na walikuwa na mitazamo potofu sana kuhusiana na Mwenyezi Mungu. Hawakutumia akili wala mantiki katika kumtambua Mwenyezi Mungu na ndio maana walitengeneza mawe na masanamu ya kila namna na kuitakidi ni miungu yao. Wanawake hawakuwa na hadhi wala heshima yoyote kwao, na waliwazika hai watoto wadogo wa kike. Lakini Bwana Mtume SAW aliivuka salama njia hiyo nzito, akawabadilisha watu hao na kuwafanya wamjue Mwenyezi Mungu wa Haki na kuwaokoa kutoka katika shimo la ukatili wa kijahilia.

Hatua ya pili ya kuzivutia nyoyo za watu ni mawaidha mazuri. Mawaidha na ukumbusho unazigeuza nyoyo ngumu kuwa laini na nyenyekevu. Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu ameshurutisha mawaidha na wema, kwa maana ya kwamba mawaidha mema ndiyo yenye taathira nzuri katika nyoyo za watu, na mawaidha mabaya maana yake ni uchochezi na kuzifanya nyoyo kuwa sugu. Hatua ya tatu katika kufanya daawa ni mijadala. Hatua hii ya tatu inawahusu watu ambao akili zao zimejaa fikra potofu na hawatengenei ila kupitia mijadala na kupambana nao kwa hoja. Ni jambo lililo wazi kwamba, mijadala inakuwa na taathira pale inaposimama juu ya msingi wa haki na uadilifu na kuwa mbali na majigambo na kujiona bora kuliko wengine. Hiyo ndiyo misingi iliyotumiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW katika kuwalingania watu Uislamu.

Mwenendo wa Mtume SAW katika Vita

Vile vile tunapaswa tuzingatie kwamba, Bwana Mtume SAW alilazimika kuingia vitani na maadui kutokana na usugu, kiburi na ukaidi wa maadui hao na kwa ajili ya kupambana na hatari ambazo zilikuwa zinawakabili Waislamu. Lakini pamoja na hayo mwenendo wa mtukufu huyo hata katika vita ulijaa huruma na uadilifu. Hakuruhusu kudhulumiwa mtu yeyote, bali alipiga marufuku kudhulumiwa hata miti na wanyama, seuze tena binadamu wasio na hatia na ambao hawapigani vita na Waislamu.
Katika kitabu cha hadith cha Biharul Anwar, Juzuu ya 19, ukurasa 177 ananukuliwa Imam Sadiq AS akisema: Kila wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa anaandaa jeshi lake kwa ajili ya kwenda vitani, alikuwa akiwaita wanajeshi wake na kuwaambia: Enendeni kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu na piganeni jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Msiibe ngawira na ghanima na wala musiifanyie shere na kuidhalilisha miili ya makafiri wanaouawa. Msiue vizee, watoto na wanawake. Msiwaue watawa walioko kwenye mapango yao na msing'oe miti na wala msichome moto mashamba. "Mushrik" yeyote atakayeomba hifadhi yenu mpeni hifadhi ili aweze kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu na muhubirieni Uislamu. Akiukubali Uislamu, huyo ni ndugu yenu katika dini na akikataa (msimdhuru bali) mpelekeni sehemu ya salama.
Naam, haya ndiyo mafundisho sahihi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na hii ndiyo sira yake iliyojaa nuru. Yeyote anayefanya ukatili na kuunasibisha na Uislamu, ukatili na jinai zake ni zake mwenyewe, na zinapingwa kikamilifu na Uislamu na sira ya mbora wa viumbe, rehema ya walimwengu, Bwana Mtume Muhammad SAW.

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha