IQNA

Wenye chuki na Uislamu wavunjia Qur'ani heshima Canada

15:50 - March 25, 2017
Habari ID: 3470906
TEHRAN (IQNA)-Watu wanaouuchukia Uislamu (Islamophobes) wameandamana na kuvunjia heshima nakala ya Qur'ani Tukufu huko Ontario, Canada mapema wiki hii.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, wahalifu hao wameipasua nakala hiyo ya Qur'ani na kutumbea juu ya kurasa walizozpasua katika mkutano wa bodi za shule huko Ontario Jumatano jioni huku wakitaka wanafunzi Waislamu wazuiwe kuswali wakiwa shuleni.

Katika kikao kilichofanyika katika Bodi ya Shule za Wilaya ya Peel mjini Ontario, wazazi walishinikiza bodi ya shule kuondoa kile walichodai kuwa wanafunzi kupewa fursa kubainisha dini katika shule. Watu 600 walitia saini waraka wakitaka wanafunzi wa shule eneo hilo kunyimwa ruhusa ya kutumia dakika 15 kila Ijumaa kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Msemaji wa bodi hiyo, Brian Woodland, amesema washiriki 80 katika kikao cha bodi hiyo walitoa matamshi makali dhidi ya Uislamu. Amekiri kuwa katika maisha yake hajawahi kuona kiwango hicho cha chuki.

Pamoja na hayo, siku ya Ijumaa bodi hiyo ilitoa taarifa na kubainisha masikitiko yake kuwa mkutano wake ulibadilika na kuwa kikao kilichojaa chuki dhidi ya Uislamu ikiwa ni pamoja na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu. Woodland amesema wanafunzi Waislamu wataendelea kuruhusiwa kutekeleza ibada zao ikiwa ni pamoja na Sala ya Ijumaa.

Kumekuwa na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu huko Canada katika miezi ya hivi karibuni. Itakumbukwa kuwa Januari 30 mwaka huu, gaidi Mkristo, mfuasi wa Rais Trump wa Marekani, aliwaua Waislamu sita katika msikiti mmoja nchini Canada.

Gaidi huyo amebainika kuwa mfuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani na alitumia bunduki aina ya AK47 aliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa katika msikiti wa Kituo cha Kiutamaduni cha Quebec, wakati wa Sala ya Ishaa.

3462454

captcha