IQNA

Magaidi wa ISIS waangamizwa Mosul, Iraq, Khilafa bandia yasambaratika

23:01 - June 29, 2017
Habari ID: 3471042
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Iraq limeyakomboa maeneo yote ya mji wa Mosul ambao ulikuwa makao ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na kwa utaratibu huo kuangamiza khilafa bandia ya kundi hilo la kitakfiri iliyokuwa imetangazwa mjini humo.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi leo ametangaza ‘kuangamia dola bandia la ISIS’ baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa magofu ya Msikiti wa Jamia wa Al Nuri, kati kati ya mji wa Mosul, msikiti ambao ulikuwa nembo ya kundi la ISIS. Ni katika msikiti huo ndipo kinara wa ISIS Abubakr al Baghdadi alitangaza khilafa yake Juni maka 2014.

Siku kadhaa zilizopita, wakati walipohisi wamezingirwa na hawana sehemu ya kutoroka, magaidi wa ISIS waliulipua msikiti huo ambao ulikuwa na mnara mashuhuri na uliojengwa miaka 1,000 iliyopita na kwa msingi huo magaidi hao wa Kiwahhabi wameharibu turathi muhimu ya Kiislamu nchini Iraq.

Baada ya jeshi la Iraq kukomboa msikiti mkuu wa al Nuri mjini Mosul, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa hivi sasa hakuna eneo lolote la Mosul lililobakia mkononi mwa ISIS.

Oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka katika makucha ya ISIS imetekelezwa na Jeshi la Iraq likishirikiana na Harakati ya Wapiganaji wa Kujitolea ambao kwa lugha ya Kiarabu ni maarufu Hashdu sh-Sha'abi.

Japokuwa yumkini mabaki ya ISIS yakaendelea kuwepo katika baadhi ya maeneo ya Iraq baada ya ukombozi kamili wa Mosul, lakini hapana shaka kuwa, kukombolewa eneo la magharibi mwa mji huo kutakuwa na maana na kumalizwa na kukomeshwa uhai wa ISIS kama kundi nchini Iraq na kulindwa ardhi yote moja ya nchi hiyo. Suala muhimu zaidi ni kuwa, uhai wa kundi la kigaidi la ISIS nchini Iraq ulianza mwezi Junimwaka 2014 na sasa harakati za kundi hilo nchini humo zimekomeshwa katika mwezi huo huo wa Juni 2017. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, mwezi wa Juni kwa Iraq ni kipindi muhimu sana, kwani wakati mwezi huo ungeweza kuhesabiwa kuwa ni mwezi wa kugawanywa nchi hiyo, sasa umekuwa zama muhimu sana za kulindwa na kuunganishwa tena ardhi ya nchi hiyo.

Operesheni ya kukomboa mji wa Mosul kama sehemu ya mwisho ya mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kiwahabi la ISIS ilianza Oktoba 2016. Kwa kuwa Mosul ulikuwa mji wa kwanza kuvamiwa na kutwaliwa na kundi hilo Juni mwaka 2014 na kuwa makao makuu ya kundi hilo nchini Iraq, hivyo operesheni hiyo inahesabiwa kuwa na umuhimu mkubwa zaidi ikilinganishwa na nyingine zilizofanyika kwa ajili ya kupambana na ugaidi.

Picha za Mabaki ya Msikiti wa Jamia wa Al Nuri uliobomolewa na ISIS

Magaidi wa ISIS waangamizwa Mosul, Iraq, Khilafa bandia yasambaratika


Magaidi wa ISIS waangamizwa Mosul, Iraq, Khilafa bandia yasambaratika


Magaidi wa ISIS waangamizwa Mosul, Iraq, Khilafa bandia yasambaratika

3613890

captcha