IQNA

Sherehe za Maulidi ya Mtume SAW katika msikiti wa kihistoria wa Al Nuri, Iraq

16:01 - October 18, 2021
Habari ID: 3474438
TEHRAN (IQNA)- Sherehe za kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad SAW maarufu kama Milad un Nabii au Maulidi zimefanyika Jumapili jioni katika msikiti wa kihistoria wa Al Nuri nchini Iraq ambao unajengwa upya baada ya kuharibiwa vibaya na magaidi wa ISIS au Daesh.

Msikiti huo wa karne ya 12 Miladia katika mji wa Mosul na amabo ni maarufu kwa mnara wake uliopinda uliharibiwa vibaya mwaka 2017 na magaidi wakufurishaji wa ISIS. Hivi sasa unakarabatiwa upya katika mradi ambao unafadhiliwa na Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO.

"Kwangu mimi ni siku ya kipekee. Nina furaha tele," amesema Marwan Muafak, 45, akiwa katika sherehe hizo.

Ameongeza kuwa, sherehe hizi ni nembo ya kurejea sauti ya maudhini na sala katika eneo hili. Wakazi wa Mosul wanataka maisha yao yarejee kama kawaida.

Mamia ya watu walikusanyika katika uwanja msikiti huo jana kuadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad SAW.

Wakazi wa Mosul wakiwa wamevalia mavazi yao ya jadi walionekana wakiwa wanapiga dufu  huku wakimsifu Mtume Muhammad Al Mustafa SAW. Sherehe hizo za Maulid zimefanyika baada ya Sala ya Ishaa.

Abu Bakr Kenaan, mkuu wa Wakfu wa Masunni katika mkoa wa Nainawa nchini Iraq amesema hii ni mara ya kwanza sherehe ya Maulid ya Mtume SAW kufanyika katika Msikiti wa Al Nuri baada ya miaka mingi. "Furaha yetu ni kubwa, ni vigumu kubainisha hisia zetu kwa maneneo wakati tunapoona watu wote hawa wakiwa wamekusanyika hapa."

Kinara wa magaidi wakufurishaji  wa ISIS au Daesh aliyeangamizwa, Abu Bakr Al Baghdadi,  alionekana mara moja tu hadharani katika msikiti huo Julai mwaka 2014 wakati alipotangaza ukhalifa wake bandia. Mwaka 2017 jeshi la Iraq lilkomboa eneo lote la kaskazini mwa Iraq na kuwatimua magaidi hao wakufurishaji.

UNESCO imekusanya dola milioni 100 hadi sasa kwa ajili ya kuukarabati msikiti huo na inatazamiwa kuwa mradi huo utakamilika mwaka 2023.

Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. 

Kwa ujumla Waislamu huadhimisha Maulidi katika mwezi mzima wa Rabiul Awwal na katika baadhi ya nchi sherehe hizo huendelea hata katika mwezi unaofuata wa Rabiu Thani.

3476093

Kishikizo: nuri ، msikiti ، iraq ، maulidi ya mtume saw
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha