IQNA

Wakaazi wa Mosul wahitaji ushauri nasaha baada ya ISIS kutimuliwa

11:52 - July 10, 2017
Habari ID: 3471058
TEHRAN (IQNA)-Baada ya serikali ya Iraq kutangaza rasmi kukombolewa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidiwa ISIS au Daesh, imebainika kuwa wakazi wa mji huo wanahitaji ushauri nasaha.

Jana Jumapili Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi aliangaza rasmi ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika mji wa Mosul miezi minane baada ya kuanza vita dhidi ya magaidi hao wakufurishaji.

Katika taarifa, Ofisi ya al-Ibadi ilisema, "Amiri Jeshi Mkuu, Waziri Mkuu Haider al-Abadi, amewasili katika mji uliokombolewa wa Mosul na kuwapongeza wapiganaji shujaa na watu wa Iraq kwa ushindi wao mkubwa."

Mwandishi wa IQNA mjini Mosul anasema magaidi wa ISIS wametimuliwa kikamilifu mjini humo ingawa yamkini kuna wachache waliojificha miongoni mwa wananchi. Aidha katika eneo la kale la mji wa Mosul kuna uharibifu mkubwa uliotekelezwa na magaidi wa ISIS na kwamba magaidi waliwatumia raia wa eneo hilo kama ngao ya binadamu ambapo idadi kubwa ya raia walipoteza maisha. Sababu ya kuchukua muda mrefu kabla ya kukombolewa Mosul magharibi ni kuwa wanajeshi wa Iraq walikuwa wanasonga mbele polepole sana ili kuzuia kupoteza maisha raia. Aidha anasema magaidi wa ISIS hawakuwa na huruma hata kidogo na walikuwa wanawaua raia na kubomoa nyumba zao kila walipokuwa wanahisi wamezingirwa.

Wanasaikolojia wanasama baada ya kukombolewa mji wa Mosul, sasa kuna haja ya kuwapa wakaazi wa mji huo ushauri nasaha kwani wameathiriwa vibaya na vita na ukaliwaji mabavu mji huo na ISIS tokea Juni mwaka 2014. Aidha wakuu wa Iraq wametakiwa kuimarisha jitihada za kuleta umoja wa kisiasa na kijamii katika mji huo ambao kabla ya kukombolewa ulikuwa mji mkuu wa khilafa bandia ya ISIS. Halikadhalika viongozi wa kidini na kisiasa Iraq wanasema baada ya kuangamizwa kijeshi ISIS, kazi kubwa itakuwa ni kutokomeza fikra na idiolojia potovu ya utakfiri ambayo chimbuko lake ni Uwahhabi. Aidha baada ya kutimuliwa ISIS mjini Mosul kuna wasiwasi kuwa magaidi wachache waliosalia wataendelea kutekeleza mashambulizi ya kuvizia nchini Iraq.

3616679/

captcha