IQNA

Washindi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Iran watangazwa

23:39 - April 25, 2018
Habari ID: 3471481
TEHRAN (IQNA)-Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Kusoma na Kuhifadhi Qur’ani Tukufu ya Iran yamemalizika rasmi Jumatano kwa kutunukiwa zawadi washindi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sherehe za kufunga mashindano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA mjini Tehran zimehudhuriwa na Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani, Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran Hujjatul Islam Ali Mohammadi na maafisa wengine wa ngazi za juu, wanazuoni na wataalamu wa Qur’ani Tukufu pamoja na washiriki wa mashindano hayo kutoka maeneo mbali mbali duniani.

Katika kategoria ya qiraa kitengo cha kawaida cha wanaume nafasi ya kwanza imechukuliwa na Ali Ridhaa Ridhai wa Afghanistan huku Sayyid Mustafa Husseini wa Iran akichukua nafasi ya pili naye Abbas Mustafa wa Lebanon ameashika nafasi ya tatu. Katika  kategoria ya kuhifadhi Qur’ani kitengo cha kawaida cha wanaume Mustafa Isfahanian wa Iran amechukua nafasi ya kwanza akifuatiwa na Mohammad Rashid wa Misri huku Ehsanullah Abulhashemi wa Bangladesh akiwa wa tatu. Katika kategoria ya Mashindano ya Pili ya Kimatiafa ya Qur’ani ya Wanawake Hakima Nasiri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amechukua nafasi ya kwanza akifuatiwa na Aqila Ben Qrush wa Algeria huku Ashura Amani Lilanga wa Tanzania akishika nafasi ya tatu.

Mashindano ya mwaka huu yaliyoafunguliwa rasmi Jumatano iliyopita yamejumuisha Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran (ya kawaida maalumu kwa ajili ya wanaume) na pia kunafanyika mashindano mengine ya Qur'ani ya wanawake, ya wenye ulemavu wa macho, ya wanafunzi wa vyuo vikuu na ya wanachuo wa vyuo vya kidini.

Mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani yamefanyika kwa kaulimbiu ya "Kitabu Kimoja, Umma Mmoja" na yalizinduliwa sambamba na kuanza sherehe za mwezi huu mtukufu wa Shaaban ambapo yamewajumuisha wasomaji (quraa)   na waliohifadhi (hufadh)  Qur'ani  258 kutoka nchi 84.

3709128

captcha