IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Msiziamini nchi 3 za Ulaya katika mapatano hadi zitoe dhamana

20:53 - May 09, 2018
Habari ID: 3471502
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria baadhi ya matamshi kuhusu Iran kuendelea kuwepo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na nchi tatu za Ulaya na kusisitiza kuwa: "Kuhusu kufanya mazungumzo na nchi tatu za Ulaya, haipaswi kuziamiani na katika kila mapatano lazima kuwepo dhamana ya kweli na ya kivitendo la sivyo haiwezekani kuendelea kwa hali iliyopo."

Msiziamini nchi 3 za Ulaya katika mapatano hadi zitoe dhamanaAyatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi alipowahutubia wanachuo na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Waalimu mjini Tehran. Ameashiria hotuba ya kishenzi na duni ya Rais Donald Trump jana usiku na kusema: "Huyu mtu mbali na kutamka nukta 10 za uongo wa wazi, pia alitoa vitisho dhidi ya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu na mimi hapa  kwa niaba ya taifa la Iran ninamwambia,  ''unachofanya wewe hakina maana.'"

Ayatullah Khamenei aliongeza kuwa: "Uadui wa Wamarekani usio na kikomo na wa kina wenye lengo la kuupindua mfumo si uadui nami binafsi au wakuu wengine wa nchi, bali wana uhasama na mfumo wa Kiislamu na taifa ambalo limeuchagua mfumo na limechukua mkondo wa mfumo huo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria visingizo vya Marekani kuhusu uwezo wa kujihami na uwepo wa Iran katika eneo na kusisitiza kuwa: "Iwapo kesho tutatangaza kuwa hatuzalishi tena makombora au kupunguza masafa ya makombora hayo suala hilo halitaishia hapo na bila shaka wataibua kisingizio na kadhia nyingine na hii ni kwa sababu mgogoro wetu nao ni wa kimsingi kwani Marekani inapinga msingi wa uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu."

Aidha amesema sababu kuu ya uhasama huu shadidi ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu jambo ambalo lilipelekea kukatwa mikono ya Wamarekani nchini Iran. Ameongeza kuwa: "Wanataka kuangamiza mfumo wa Kiislamu ili kwa mara nyingine waweze kuitawala Iran, nchi ambayo ina hifadhi muhimu ya maliasili na umuhimi wa kistratijia."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Wamarekani wanataka watumwa ambao, sawa na baadhi ya watawala wa nchi za eneo, watakuwa wakiwatii kikamilifu lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na taifa la Iran litadumisha nguvu na uwezo wake mbele yao na hawawezi kustahamili adhama hii."

Ayatullah Khamenei ameashiria barua ambayo hivi karibuni Trump aliwaandikia watawala wa nchi za Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa: "Rais wa Marekani katika barua ya nchi hizo aliziamuru zifanye hili na lile." Amesema Wamarekani wanataka mfumo wa Kiislamu uwe kama nchi hizo za Kiarabu lakini hawawezi kufanikiwa kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebadilisha udhalilishaji wa taifa na nchi katika zama za wafalme wa Qajar na Pahlavi kuwa ni izza, uhuru na kusimama kidete.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema muamala mchafu na duni wa Trump ulitarajiwa na kuongeza kuwa: "Wale ambao walikuwa na uhasama na taifa la Iran sasa mifupa yao iko chini ya ardhi lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara."

3712872

captcha