IQNA

Wajue Waislamu Waafrika waliofikisha Uislamu Marekani

13:05 - August 29, 2018
Habari ID: 3471651
TEHRAN (IQNA)- Leo idadi ya Waislamu Marekani wanakadiriwa kuwa karibu milioni tatu na nusu lakini wengi hawajui ni kuwa Waafrika ndio waliokuwa miongoni mwa Waislamu wa kwanza katika nchi hiyo.

Waislamu hao walifika Marekani katika zama za biashara ya utumwa na aghalabu walikuwa wanajua kusoma na kuandika Kiarabu kwani walitoka eneo la Afrika Magharibi ambalo lilikuwa kitovu cha Uislamu.  Kuna mifano kadhaa ya Waislamu Waafrika waliofikisha Uislamu Marekani na miongoni tunaweza kuwataja Bilali Muhmmad, Ayub Job Djalli, Yarro Mamood, Ibrahim Abdulrahman ibn Sori, Ummar ibn Sayyid na Sali Bilali. Wote hao walifika Marekani kama watumwa.

Bilali Muhammad

Alizaliwa mwaka 1770 katika eneo la Afrika ambalo leo linajulikana kama Guinea na Sierra Leone na alikuwa miongoni mwa vigogo wa kabila la Fulani. Alikuwa anazungumza lugha ya Kiarabu mbali na kuwa mtaalamu wa hadith, tafsir na masuala ya sheria za Kiislamu. Bilal aliandika makala ya kurasa 13 kuhusu sheria za Kiislamu kwa mujibu wa madhehebu ya Imam Malik na alimzawadia rafiki yake kabla hajaaga dunia. Wengi walidhani makala hiyo ilikuwa ni kumbukumbu za maisha kabla ya kupelekwa katika Chuo Kikuu cha Al Azhar na kubainika kuwa ilikuwa makala ya fiqhi.

Ayuba Suleiman Diallo

Alizaliwa katika Senegal ya leo katika familia iliyoheshimika ya Fulbe na jina lake la utumwa lilikuwa Job Ben Solomon. Aliandika kumbukumu za maisha yake akiwa kama mtumwa katika jimbo la Maryland kwa miaka kadhaa.  Inasemekana aliuzwa kama mtumwa kimakosa na hatimaye alifanikiwa kurejea nchini Senegal akiwa bado ni Mwislamu. Alikuwa hafidh wa Qur'ani Tukufu na kuna nakala ya Qur'ani  kwa mkono wake nakala ya Qur'ani Tukufu.

Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Ayub bin Suleiman alikuwa Imamu wa msikiti kabla ya kutekwa nyara na Wazungu waliokuwa wakifanya biashara ya utumwa.

Yarrow Mamout

Alizaliwa katika Guinea ya leo mwaka 1736 na alifariki mwaka 1823 akiwa huru baada ya kuwa mtumwa kwa miaka kadhaa. Alifika Maryland Marekani akiwa na umri wa miaka 14 akiwa ameandamana na dada yake. Mamout alikuwa anafahamu lugha ya Kiarabu na alizingatia mafundisho ya Kiislamu maishani hadi kifo chake.

Abdulrahman Ibrahim ibn Sori

Alizaliwa katika Guinea ya leo na alitambuliwa kama mwanamfalme miongoni mwa watumwa kwani alikuwa mwana wa Mfalme Sori wa kijiji cha Timbo. Abdulrahman alikuwa kamanda wa kijeshi na alikamatwa katika shambulizi la kuvizia na kupelekwa hadi eneo la Mississippi nchini Marekani. Alioa na kupata watoto na kufanya kazi kwa muda wa miaka 40 kabla ya kuachiliwa huru. Alifariki akiwa njia kurejea katika nchi yake. Aliwahi kuiandikia barua familia yake Afrika kwa lugha ya Kiarabu. Inadokezwa kuwa barua hiyo ilifika mikononi mwa Sultan Abderrahmane wa Morocco na aliguswa sana na yaliyomo kiasi cha kumaundikia barua Rais John Quincy Adams ili amuachilie huru.

Ummar bin Sayyid

Alizaliwa eneo la Futa Tooro nchini Senegal mwaka 1770 na alikamatwa na wauza watumwa mwaka 1807 na alifahamika baadaye kwa majina ya Omar Moreau na Prince Omeroh. Alitambulika kama msomi wa Uislamu mbali na kuwa mtaalamu wa hisabati ambapo aliandika makala kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.

Sali Bilali

Sali Bilali alizaliwa Mali yae leo na alitekwa na kufanywa mtumwa mwaka 1782 na inaarifiwa kuwa maneneo yake ya mwisho yalikuwa ni shahada mbili.

Kwa msingi huo Waislamu wenye asili ya Afrika wamekuwa na nafasi kubwa katika kueneza Uislamu nchini Marekani. Hivi sasa nchini Marekani kuna vuguvugu maarufu ya Waislamu wenye asili ya Afrika maarufu kama, Nation of Islam.

captcha