IQNA

21:11 - November 20, 2019
News ID: 3472224
TEHRAN (IQNA)- Waislamu duniani wameendelea kulaani hatua ya Marekani kubadili msimamo na kuanza kuunga rasmi hatua iliyo kinyume cha sheria ya Israel ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza kuwa nchi yake imebatilisha sera yake ya miongo minne na kudai kuwa, kitendo cha Israel cha kujenga vitongoji vya Walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina 'si kinyume cha sheria za kimataifa'.

Pompeo ambaye aliwahi kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la CIA amedai uamuzi huo unalenga kuunga mkono sera za Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) ambazo zimetungwa na Jared Kushner, Yahudi-Zayuni ambaye ni mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani .

Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimesema  hatua hiyo ya Marekani ni ukiukwaji wa wazi wa haki za Wapalestina. Al Azhar imesema taarifa hiyo ya Pompeo inakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo imeashiria pia sera mbovu za Marekani kuhusu Palestina, hasa kuutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Al Azhar imetoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu katika kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel.

Wakati huo huo Baraza la Mashauriano ya Taasisi za Kiislamu Malaysia limelaani vikali tangazo hilo la Marekani kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mkuu wa baraza hilo Mohammad Azmi Abdul amesema uamuzi huo wa Marekani ni sawa na kuunga mkono jinai za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina. Ameitaja kuwa ya kishetani sera hiyo ya Marekani ya kuupa sura ya kisheria uporaji wa ardhi za Palestina unaotekelezwa na Israel ili kuwaruhusu Mayahudi kujenga vitongoji haramu vya Kizayuni.

Wakati huo huo, Palestina imelalamikia uungaji mkono wa Marekani kwa ujenzi haramu wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo  wa Magharibi wa Mto Jordan kwa kuuandikia barua tatu Umoja wa Mataifa. Riyadh Mansour, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa leo amewasilisha barua tatu kwa umoja huo na kulaani hatua mpya iliyochukuliwa na Washington ya kuunga mkono ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Katika barua hizo, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amelalamikia misimamo iliyotangazwa hivi karibuni na viongozi wa Marekani kuhusu uungaji mkono wa Washington kwa upanuzi wa vitongoji unaofanywa na Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.

Barua hizo zimewasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Baraza la Usalama na Rais wa Baraza Kuu la umoja huo.

Uungaji mkono wa Marekani kwa ujenzi haramu wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina umelalamikiwa na kukosolewa na Wapalestina wenyewe, nchi kadhaa za Kiislamu zikiwemo Iran na Misri na pia Umoja wa Ulaya.

Tarehe 23 Desemba mwaka 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 2334 la kuutaka utawala wa Kizayuni wa Israel usimamishe kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika maeneo ya makazi ya Wapalestina.

38583503469927

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: