IQNA

19:52 - November 23, 2019
News ID: 3472227
TEHRAN (IQNA) – Kituo cha Kimataifa cha Fatwa katika Chuo cha Al Azhar nchini Misri kimetoa taarifa na kusema vazi la Hijabi ni faradhi kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

Taarifa ya kituo hicho imetaja aya ya 21 katika Sura An-Nuur na aya ya 59 katika Sura Al Ahzab na kusema ni  sura ambazo zinaashiria kuwa ni lazima au ni faradhi kwa wanawake Waislamu kuvaa vazi la staha la Hijabu.

Kituo cha Kimataifa cha Fatwa katika Chuo cha Al Azhar kimebaini katika taarifa hiyo kuwa: "Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu na istidlali ya Wahyi, Hijabu ni wajibu na hili si suala la kufanyiwa Ijtihadi  na wala hakuna yeyote mwenye haki ya kupingana na hukumu hii thabiti na ya yakini ya Qur'ani Tukufu.

Taarifa hiyo imetahadharisha kuhusu kuenezwa baadhi ya madai kuwa eti Hijabu si faradhi na kuongeza kuwa: "Watu wasio wataalamu na wa kawaida hawapaswi kujiingiza katika suala hili."

Taarifa ya Kituo cha Kimataifa cha Fatwa katika Chuo cha Al Azhar nchini Misri imeendelea kwa kutaja aya za Qur'ani Tukufu ambazo zina dalili za wazi zinazoonyesha kuwa Hijabu ni wajibu kwa wanawake na kusema; Mwenyezi Mungu SWT katika sehemu ya Aya ya 31 ya Surat An-Nur ya Qur'ani Tukufu anasema: "Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao…" Aidha Mwenyezi Mungu SWT katika Aya ya 59 ya Surat Al Ahzab anasema: "Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu."  Kituo cha Kimataifa cha Fatwa katika Chuo cha Al Azhar kimesema aya hizo mbili zinabainisha wazi kuhusu kuwa ni wajibu kuvaa Hijabu kwa wanawake Waislamu.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Iwapo mtu atalitazama suala la Hijabu kwa insafu na uadilifu, basi itambainikia kuwa vazi hili la Kiislamu ni kwa maslahi ya mwanamke na linaendana na maumbile ya mwanadamu kabla hata ya kuwa ni amurisho la kidini".

Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni nchini Misri, suala la kufaradhishwa vazi la Hijabu limeibua mjadala mkali ambapo baadhi ya wasanii na wanahabari nchini humo wametaka Hijabu ipigwe marufuku nchini humo.

3858687

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: