IQNA

Baraza Kuu la UN lailaani Myanmar kwa kuwandamiza Waislamu Warohingya

18:52 - December 28, 2019
Habari ID: 3472309
TEHRAN (IQNA) - Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Ijumaa limepasisha azimio ambalo linailaani vikali Myanmar kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na jamii za wengine waliowachache katika nchi hiyo ya Mabuddha.

Katika azimio katika baraza hilo lenye wanachama 193, nchi 134 ziliunga azimio hilo, nchi tisa zilipinga na 28 hazikupiga kura. Azimio hilo pia linaitaka Myanmar ichukue hatua za dharura kukabiliana na chuki dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na jamii zingine za waliowachache katika majimbo ya Rakhine, Kachin na Shan.

Utawala wa Myanmar unawatazama Waislamu Warohingya kuwa ni 'Wabengali' kutoka nchi jirani ya Bangladesh pamoja na kuwa wamekuwa nchini humo kwa karne kadhaa.

Ikumbukwe kuwa, Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, mwezu huu ilianza kusikiliza faili la kesi ya mauaji ya umati yaliyofanywa na wanajeshi wa Myanmar mwaka 2017 dhidi ya Waislamu Warohingya ambayo iliwasilishwa katika mahakama hiyo na serikali ya Gambia kwa niaba ya nchi 57 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

3470199

captcha