IQNA

Waislamu Warohingya wanakabiliwa na baa la njaa

12:19 - April 19, 2020
Habari ID: 3472681
TEHRAN (IQNA) – Sheria ya kutotoka nje ili kuzuia kuenea ugonjwa wa corona nchini India imepelekea Waislamu wa jamii ya Rohingya wasiweze kupokea msaada wa chakula kutoka kwa wahisani na hivyo wanakabiliwa baa la njaa.

Waislamu hao Warohingya ambao wametoroka nchi yao, Myanmar, kutokana na hofu ya kuuawa, wako katika kambi zilizoko New Delhi na Jamu na Kashmir.

Wakati huo huo makumi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wamepoteza maisha kutokana na njaa baada ya boti yao kukwama baharini kwa majuma kadhaa.

Gadi ya Pwani ya Bangladesh ilisema jana Alkhamisi kuwa, boti hiyo iliyokuwa ikielekea Malaysia, ilikwama na kuelea katikati ya bahari kwa muda wa miezi miwili na ilifika kwenye ufuo wa bahari siku ya Jumatano baada ya kusukumwa na mawimbi.

Taarifa ya Gadi ya Pwani ya Bangladesh imesema zaidi ya Warohingya 24 wamepoteza maisha katika tukio hilo, lakini 382 walionusurika watarejeshwa Myanmar, walikokimbia mauaji na ukatili wa maafisa usalama wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Februari mwaka huu, Waislamu 16 wa jamii ya Rohingya walifariki dunia baada ya boti yao kuzama katika Pwani ya Bengal, kaskazini mwa Bangladesh.

Waislamu wa Myanmar wanaume kwa wanawake pamoja na watoto wadogo wamekuwa wakifariki dunia mara kwa mara katika matukio ya kuzama boti wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya Myanmar dhidi ya jamii hiyo.

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh huku wengine wakipata hifadhi katika nchi kama vile India, Thailand na Malaysia.

3892528

captcha