IQNA

18:40 - February 01, 2020
News ID: 3472430
TEHRAN (IQNA) – Iwapo Waislamu nchini Marekani wanataka 'kuonekana' na masuala yao yazingatiwe katika ngazi za maamuzi muhimu, basi wanapaswa kushiriki katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo.

Huo ndio uliokuwa ujumbe wa mbunge katika Bunge la Kongresi la Marekani Bi. Ilhan Omar wakati alipowahutbia Waislamu katika mji wa Des Moines jimboni Iowa.

Omar ameyasema hayo alipozungumza katika Msikiti wa Jumuiya ya Waislamu mjini humo baada ya sala ya Ijumaa, siku tatu kabla ya kuanza mchujo wa kumteua mgombea wa urais wa  chama cha Democrat katika jimbo la Iowa.

Omar, ambaye anamuunga mkono Bernie Sanders kupeperusha bendera ya Wademocrat, amemtaka seneta hiyo kuwa mtetezi wa uadilifu wa kijamii.  Ilhan Omar ametoa wito kwa Waislamu kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika upigaji kura wa mchujo wa chama cha Democrat huku akisisitiza kuwa Waislamu na wahajiri ni wadau muhimu katika uchaguzi. "Uchaguzi huu unatuhusu sisi. Uchaugzi huu unawashusu mabinti zenu walioshuleni na ambao wanakabiliana na chuki dhidi ya wageni, ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu," alisema Omar mwenye asili ya Somalia.

Akihutubia umati mkubwa wa Waislamu Omar aliongeza kuwa: "Mabinti zenu hawana usalama wanapovaa Hijabu, kwa hivyo uchaguzi huu unatuhusu. Huu ni uchaguzi unaowahusu baba zetu ambao wanalazimika kufanya kazi mbili au tatu ili kuweka chakula juu ya meza."

Jimbo la Iowa lina idadi kubwa ya Waislamu na lina moja ya misikiti mikongwe zaidi Marekani.

Mbunge mwingine wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani, Bi Rashida Tlaib, mwenye asili ya Palestina naye pia ametangaza kumuunga mkono Sanders.  Waarabu na Waislamu Marekani wanamuunga mkono Sanders kutokana na kile wanachosema ni misimamo yake ya wastani kuhusu kadhia ya Palestina na sera zake za kigeni zinazopinga uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi zingine.

Ihlan alikuwa mkimbizi baada ya vita kuibuka Somalia ambapo alikimbilia nchi jirani ya Kenya na kuishi na familia yake katika kambi la wakimbizi ya Dadaab akiwa na umri wa miaka 8 kuanzia mwaka 1991 hadi 1995 kabla ya kuhamia Marekani.

3875534

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: