IQNA

Kesi ya Sheikh Zakzaky yaakhirishwa kutokana hali yake kuwa mbaya kiafya

20:18 - February 07, 2020
Habari ID: 3472448
TEHRAN (IQNA) - Kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mkewe iliyokuwa ianze kusikilizwa jana imesogezwa mbele kutokana na hali mbaya ya afya zao iliyowafanya washindwe kufika mahakamani.

Baada ya hakimu wa faili hilo pamoja na mawakili wa pande mbili kuwasili jana mahakamani tayari kwa ajili ya kuanza kesi hiyo, Femi Falana wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat alisimama na kuitaka mahakama iakhirishe kesi hiyo hadi wakati mwingine, kwani wateja wake hawawezi kufika mahakamani kutokana na afya zao kuwa mbaya.

Wakili huyo alisema: Hali za wateja wanguu ni mbaya na hasa mke wa Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye hawezi hata kutembea, hivyo naiomba mahakama iakhirtishe kesi hii.

Hakimu alimuuliza wakili huyo kama wateja wake wangeweza kufika mahakamani leo, lakini alijibu kwa kusema kwamba, hawataweza kwani wanaumwa sana.

Baada ya mashauriano hakimu aliakhirisha kesi hiyo na kutangaza tarehe 24 na 25 za mwezi huu wa Februari kama siku za kusikilizwa tena kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, (66) na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.

Wanaharakati na wapigania haki katika maeneo mbalimbali ya dunia wanaendelea kuitaka serikali ya Rais Muhamadu Buhari imuachilie huru Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe.

3877138

captcha