IQNA

17:17 - February 18, 2020
News ID: 3472482
TEHRAN (IQNA) – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amenukulu aya ya Qur'ani Tukufu kuhusu wakimbizi na akazipongeza Iran na Pakistan kutokana na ukarimu wao katika kuwapa hifadhi wakimbizi wa Afghanistan.

Guterres ameashiria aya ya 6 ya Surah al Tawba katika Qur'ani Tukufu na kuitaja kuwa yenye maelezo bora Zaidi kuhusu kuwalinda wakimbizi katika historia ya dunia.

Aya ambayo Gutteres ameashiria inasema: "Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu."

Guterres alikuwa akizungumza Jumatatu katika Mkutano wa Wakimbizi mjini Islamabad Pakistan ambapo ametoa wito wa kuwepo mshikamano na misaada zaidi kwa wakimbizi. Amezipongeza nchi za Kiislamu, hasa Iran na Pakistan, kwa kuwakaribisha wakimbizi kwa ukarimu mkubwa. Nchi 30, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimehudhuria kikao hicho cha Islamabad.

Raia milioni 2.7 wa Afghanistan wamesajiliwa rasmi kuwa ni wakimbizi walioko maeneo mbalimbali duniani ambapo milioni 1.4 kati yao hao wanaishi nchini Pakistani. Kuna idadi kubwa ya raia wa Afghanistan ambao si wakimbizi rasmi na wengi pia wanaishi Iran na Pakistan.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) , kuna wakimbizi rasmi waliojisajili wa Afghanistan wapatao milioni moja wanaoishi nchini Iran. Kuna wakimbizi wengine wapatao milioni mbili wanaoishi Iran kinyume cha sheria, au kwa ibara nyingine bila ya kuwa na nyaraka rasmi za serikali.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijasita hata siku moja kuhudumia na kuwapa mahitaji ya dharura wakimbizi hao wote. Dikri aliyoitoa  Ayatullah Khamenei, Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo mwezi Mei 2015 kuhusiana na kupewa elimu wanafunzi wa wakimbizi wote wa Afghanistan, wakiwemo wakimbizi haramu, wanaoishi nchini bila ya kuwa na nyaraka rasmi, inachukuliwa kuwa moja ya siasa bora zaidi za kuwahudumia wakimbizi duniani. Dikri hiyo inasema: 'Hakuna mtoto yeyote wa Kiafghani, hata yule anayeishi nchini Iran bila ya kuwa na nyaraka rasmi, anapasa kunyimwa masomo, na wote hao wanapasa kusajiliwa katika shule za Kiirani.'

3879581

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: