IQNA

Oparesheni za ulipizaji kisasi za vikosi vya Yemen dhidi ya Saudia

18:53 - February 22, 2020
Habari ID: 3472495
TEHRAN (IQNA) - vikosi vya jeshi la Yemen vimefanya mashamblizi mengine ya kulipiza kisasi kwa kutumia makombora dhidi ya taasisi za shirika kubwa zaidi la mafuta la Saudi Arabia la Aramco katika mkoa wa Madina, magharibi mwa Saudia.

Msemaji wa Majeshi ya Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree jana Ijumaa aliwahutubia waandishi wa habari katika mji mkuu Sana'a na kusema kuwa, vikosi vya makombora na ulinzi wa anga vya jeshi la nchi hiyo vimetekeleza operesheni iliyopewa jina la "Operesheni ya Tatu ya Mlingano" na kupiga kwa makombora taasisi za mafuta na vituo vingine muhimu vya Aal-Saud katika mji wa bandari wa Yanbu, yapata kilomita 165 magharibi mwa Madina.

Amesema makombora ya balestiki ya Yemen yamelenga kwa shabaha maeneo yaliyokusudiwa na kuisababishia hasara kubwa serikali ya Riyadh.

 Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema mashambulizi hayo ya vikosi vya Yemen dhidi ya taasisi za mafuta za Saudia ni muendelezo wa operesheni za ulipizaji kisasi kwa uvamizi na hujuma za muungano wa Saudia dhidi ya taifa hilo la Kiarabu. 

Vikosi vya Yemen vimetekeleza mashambulizi hayo siku chache baada ya Wayemen zaidi ya 30 wakiwemo watoto 19 kuuawa katika mashambulizi ya anga ya Februari 15 yaliyofanywa na ndege za kijeshi za muungano vamizi wa Saudia katika mkoa wa Jawf, kaskazini mwa Yemen. 

Yahya Sarie amesisitiza kuwa jeshi la Yemen litaendeleza mapambano hadi litakapofanikiwa kukomboa ardhi yote ya nchi hiyo na kuwafukuza kikamilifu wavamizi wa kigeni. 

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

3880427

captcha