IQNA

Maandamano yafanyika Marekani kulaani mauaji ya Waislamu India

11:38 - March 01, 2020
Habari ID: 3472517
TEHRAN (IQNA)- Watu wa Marekani wenye asili ya India wameandamana katika miji mikubwa ya Marekani kulaani mauaji ya makumi katika ghasia za kupinga sheria mpya ya uraia nchini India.

Nje ya ubalozi mdogo wa India mjini New York, waandamanaji hao walisikika wakiwazomea na kupiga nara ya 'fedheha!' kwa maafisa waliokuwa wakiingia na kutoka kwenye ubalozi huo.

Sana Qutubuddin, mwanaharakati wa Muungano wa Haki na Uwajibikaji alihutubia mkusanyiko wa waandamanaji mjini New York na kusema, "tumechoka!"

Mbali na muungano huo, mashirika mengine yaliyoshiriki maandamano ya Ijumaa jioni katika miji mbalimbali ya Marekani ni Baraza la Waislamu Wahindi wa Marekani, South Asia Solidarity Initiative na Equality Labs.

Sambamba na kulaani ghasia zilizosababishwa na sheria tata yenye kuwabagua Waislamu katika mji mkuu wa India, New Delhi, waandamanaji hao nchini Marekani wameitaka serikali ya New Delhi inayoongozwa na Waziri Mkuu Narendra Modi ifute sheria hiyo mara moja.

Watu 42 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika ghasia hizo zinazotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kuikumba India katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.

Sheria hiyo tata inaruhusu kupewa uraia wahajiri wasio Waislamu waliokimbilia India kutoka nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan, huku ukiwanyima haki hiyo ya uraia Waislamu.

3470790

captcha