IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wa Nairuzi*
12:17 - March 20, 2020
News ID: 3472584
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mwaka mpya wa Kiirani wa 1399 Hijria Shamsia ulioanza leo nchini Iran kuwa ni Mwaka wa Ustawi Mkubwa katika Uzalishaji na kusema: Hatua kubwa ya uzalishaji inapaswa kuleta mabadiliko yanayohisika katika maisha ya wananchi.

Katika ujumbe huo wa Nowruz au Nairuzi uliotolewa leo Ijumaa kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameashiria tukio la kusadifiana mwanzo wa mwaka na siku ya kuuliwa shahidii Imam Mussa al Kadhim (as) na akamtumia sala na salamu za Mwenyezi Mungu mtukufu huyo. Vilevile amewapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kupewa utume na kubaadhiwa Nabii Muhammad (saw) katika siku hizi za mwishoni mwa mwezi wa Rajab. Vilevile amelipa mkono wa kheri ya mwaka mpya wa Nowruz taifa la Iran hususan familia za mashahidi, vilema wa vita, wanajihadi wanaotoa huduma katika medani ya afya na wafanyakazi wote wanaofanya bidii kote nchini. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezipa mkono wa pole na vilevile kuzipongeza familia za mashahidi wa mwaka uliopita wa 1398 Hijria Shamsia hususan Shahidi Qassem Soleimani, Abu Mahdi al Mohandes na wenzao na kuutaja mwaka uliopita kuwa ulikuwa mwaka uliojaa misukosuko mingi kwa taifa la Iran. Amesema kuwa, mwaka uliopita ulianza kwa mafuriko na umemalizika kwa virusi vya corona, na katika kipindi chote cha mwaka huo kumejitokeza matukio mengi kama mitetemeko ya ardhi, na vikwazo na kwamba kilele cha matukio hayo ni jinai ya kigaidi iliyofanywa na Marekani ya kumuua shahidi kamanda mashuhuri wa Iran na Uislamu, Haj Qassem Soleimani.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwaka uliopita wa 1398 Hijria Shamsia ulikuwa na mitihani migumu. Amesisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kufika popote kwa kuzama katika anasa na raha na kuongeza kuwa: Kuyashinda mashaka na kuyavuka kwa ushujaa kunalifanya taifa kupata nguvu, hadhi na heshima, kama ambavyo hadi sasa taifa la Iran limeweza kuvuka matatizo kwa njia hiyo na litaendelea kuyashinda. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran sambamba na madhara yake, vimekuwa pia na faida na vimetulazimisha kutayarisha na kutengeneza vifaa na mahitaji yetu hapa nchini kupitia suhula za ndani ya nchi, na harakati hii itaendelea kwa matakwa yake Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, mwaka uliopita ulikuwa mwaka mgumu na wa wenye mashaka kwa wananchi lakini sambamba na mashaka hayo ulikuwa pia na mafanikio ambayo baadhi hayajawahi kushuhudiwa; na taifa la Iran kwa hakika liling'ara nas kufanya vizuri.

Amesisitiza tena kuwa mwaka huu mpya ni mwaka wa harakati kubwa ya uzalishaji na kuwataka maafisa wa serikali kufanya kazi kwa namna ambayo italeta mabadiliko yanayohisika katika maisha ya wananchi. 

*Inafaa kukumbusha hapa kuwa, leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz au Nairuzi. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz.

Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

3886557

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: