IQNA

Rais Hassan Rouhani katika ujumbe wa Nairuzi*

Mwaka 1399 Hijria Shamsia uwe mwaka wa afya, ajira na ustawi wa uchumi Iran

12:10 - March 20, 2020
Habari ID: 3472583
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Iran ametuma ujumbe wa munasaba wa mwaka mpya wa Kiirani wa 1399 Hijria Shamsiya na kusema mwaka mpya utakuwa mwaka wa afya, ajira na ustawi wa kiuchumi na kiutamaduni nchini Iran.

Rais Rouhani aidha ameongeza kuwa,  mwaka uliopita ulikuwa mwaka wa matukio na hamasa nyingi, na kwamba matukio makubwa zaidi katika historia ya nchi hii na hamasa zenye fahari kubwa zimetengenezwa na wananchi mashujaa wa Iran katika mwaka huo.
Katika ujumbe wake wa Nowruz au Nairuzi, Rais Rouhani amezungumzia vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa: Maadui wa Iran wametekeleza vikwazo shadidi zaidi wakidhani kwamba, wananchi watasalimu amri lakini taifa kubwa la Iran limesimama kidete mbele ya mashaka hayo na kutengeneza hamasa ya idara madhuburi ya uchumi usiotegemea mafuta ambayo imetimia kwa mara ya kwanza hapa nchini katika miongo kadhaa ya hivi kariibuni. 
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameongeza kuwa, Wamarekani walitaka kuitumbukiza Iran katika hali ya mgogoro kwa kuzidisha mfumuko wa bei na mgogoro wa uchumi, lakini kinyume chake, takwimu zote zinaonyesha kuwa, uchmi wa Iran ulikuwa na kuimarika katika miezi 9 ya  mwaka uliopita, na mfumuko wa bei umedhibitiwa kwa kiwango kikubwa. 
Rais Rouhani amesema: Hii leo katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia akiba ya kistratijia ya Iran iko katika hali bora zaidi kuliko miaka iliyopita.
Ameongeza kuwa: Iran haijashindwa, imesimama kidete mbele ya mashinikizo ya Marekani na imeishinda Washington katika Mahakama ya Kimataifa, na kuinuka kifua mbele na kushinda katika duru zote za kimataifa na fikra za walimwengu katika upande wa masuala ya kisiasa. 
Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Rais Rouhani amewashukuru wafanyakazi wa sekta ya tiba nchini, hasa madaktari na wauguzi kwa kazi yao kubwa katika ukukabiliana na kirusi cha corona au COVID-19.
 
*Inafaa kukumbusha hapa kuwa, leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz au Nairuzi. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.
 
captcha