IQNA

Waziri wa Ulinzi wa Sudan afariki akiwa katika mazungumzo ya amani

12:17 - March 25, 2020
Habari ID: 3472599
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Luteni Jenerali Jamaleldin Omar, amefariki baada ya kupata mshtuko wa moyo akiwa Sudan Kusini katika mazungumzo ya amani baina ya serikali na waasi mjini Juba.

Katika taarifa siku ya Jumatano, Jeshi la Sudan limesema, Omar alikuwa mwanachama wa baraza la kijeshi lilolochukua madaraka baada ya kupinduliwa Omar al Bashir mwaka uliopita.

Imedokezwa kuwa, Omar alishiriki katika mazungumzo yaliyoendelea hadi Jumanne usiku na aliaga dunia usiku wa kuamkia leo. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu kifo cha waziri hiyo.

Mazungumzo ya wawakilishi wa serikali ya Sudan na viongozi wa makundi ya waasi yalianza upya katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba Oktoba mwaka jana.

Mazungumzo hayo ya amani yalianza kufuatia mwito wa nchi za eneo kwa pande hizo kuonyesha nia ya kisiasa ya kutatua mgogoro ambao umekuwa ukitokota nchini humo kwa muda mrefu.

3887304

captcha