Kwa mujibu wa tovuti ya Al-Masirah, baba, mkewe mjamzito na watoto wao wawili wameuawa katika shambulizi hilo la kikatili baada ya nyumba yao kulengwa na roketi la Saudia katika eneo la BeniSayyah, wilaya ya Razih mkoani Sa'ada.
Mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi mwa Yemen mpakani mwa Saudia umekishambuliwa karibu kila siku na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh, ambapo mbali na raia kuuawa, lakini pia miundimsingi ya mkoa huo imeharibiwa vibaya na hujuma hizo za anga.
Jana vyombo vya habari vya Yemen viliripoti kuwa, muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umetekeleza mashambulio 19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al-Masirah, maeneo yaliyoandamwa na mashambulio ya vikosi vamizi vinavyoongozwa na Saudi Arabia ni Sa'adah, Ma'rib, Imran na Hajjah.
Hivi karibuni kituo cha Haki za Binaadamu cha Ain Al-Insaniyah kilielezea kuuawa na kujeruhiwa zaidi ya Wayemen 42,000 katika kipindi cha miaka sita ya uvamizi na mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia.
Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.